STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
20.4.2016
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali
itahakikisha inawapelekea huduma zote muhimu wananchi waliaothirika na mvua za
masika na hakuna hata mmoja atakae kaa
na njaa kwa kukosa chakula.
ameyasema
hayo mara baada ya kuwatembelea wananchi walioathirika na mvua za masika
zinazoendelea hapa nchini ambao wanaoishi kwa muda katika kambi ya skuli ya
Mwanakwerekwe C.
Dk. Shein mesema
kuwa hatua hizo za kuwahudumia wananchi wake ni wajibu wa Kikatiba kwa kutakiwa
waishi vizuri sambamba na kupata huduma zote za msingi kwa kuenziwa wao pamoja
na mali zao.
Katika
mazungumzo yake na wananchi hao Dk. Shein ametumia fursa hiyo kuwawapa pole kwa
matukio yaliowatokezea na kueleza kuwa hizo zote ni rehema za MwenyeziMungu na
wanatakiwa kuzipokea kwa nguvu zote huku akiahidi kuwa Serikali yao itaendelea
kuwasaidia.
“Kufanya
hivyo ni wajibu wa Serikali kwani kama tungekuwa na uwezo wa kila mtu kumpa
nyumba yake tungempa lakini uwezo hatuna lakini hata hivyo tutahakikisha
Serikali inafanya kila iwezekanavyo kukufanyieni yale yote yanayowezekana”,amesema
Dk. Shein.
Aidha, Dk.
Shein amesema kuwa kuanzia leo Serikali itahakikisha kwa yale yote yaliyokuwa
hayapo wanapelekewa ikiwa ni pamoja na kuwapekea TV ili waweze kupata taarifa
za nchi yeo huku akiwahakikishia wananchi hao kuwa watoto wote wanaosoma skuli
ambao wapo katika kambi hiyo kuanzia leo watapelekwa skuli.
Dk. Shein
amesema kuwa matukio hayo yote ya mafuriko yaliosababishwa na mvua za masika ni
matokeo ya mabadiliko ya mji wa Zanzibar hivi sasa ambao katika baadhi ya
maeneo hayakujengwa kwa kufuata taratibu za ujenzi na ndipo zinazonyesha mvua
kubwa husababisha maafa makubwa.
Amesema
kuwa ujenzi uliojengwa wa kutofuata mipango miji ndio uliopelekea kuifanya
Zanzibar hata kutokuwepo kwa utaratibu wa maji ya mvua kufuata mitaro ambayo
kwa hivi sasa miundombinu ya kutoa maji ya mvua nayo haipo hali ambayo
huchangia kutokea kwa mafuriko.
Dk. Shein
ameeleza kuwa athari hizo pia, husababishwa na baadhi ya watu wenye uwezo wa
kifedha ambao wamezizungushia nyumba zao makuta ambayo huzuia maji na
kusababisha maji kutuama na hatimae kuleta athari.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein amesema kuwa makaazi hayo katika kambi hiyo ni kwa muda tu
kutokana na maafa yaliowatokezea wananchi hao lakini hata hivyo Serikali
itahakikisha mara baada ya maeneo yao kuanza kukalika yanakuwa katika hali
nzuri na ndipo waweze kuanza tena maisha.
Kwa upande
mwengine Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya maafa yaliotokea baada ya kunyesha
mvua za masika yakiwemo mafuriko pia, mvua hizo zimepelekea kuongezeka kwa
maradhi ya kipindipindu na kuwataka wananchi kufuata maelekezo wanayopewa na
taasisi husika katika kujikinga na maradhi hayo.
“Wananchi msifanye mas-hara, tukumbuke mwaka
1978 yalipoibuka kwa kasi maradhi haya...hakuna hata Wilaya moja isiyokuwa na
kipindupindu hivi sasa...wananchi mfuate taratibu msiwe wakaidi mkiambiwa
msiuze biashara zilizokatatwa msiuze, unadhifu upewe kipaumbele”,amesisitiza
Dk. Shein.
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo, kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kupitia Idara yake ya Maafa kwa juhudi
wanazozichukua katika kuwapa huduma za lazima wananchi hao ambao nao uongozi
huo kwa upande wake ulimuhakikishia Rais kuwa wamejipanga vizuri kutoa huduma
stahiki kwa wahanga hao wote.
Wananchi
wapatao 420 wapo kwenye kambi hiyo wakiwemo wanawake 240 na wanaume 180 ambapo
watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano wapo 54 na wazee wa miaka 60
hadi 70 wapo 62, hao wote wanatoka katika Shehia za Kwahani, Welezo na Nyerere
katika Wilaya ya Mjini Unguja.
Wakati huo
huo, Dk. Shein alitembelea kambi ya kipindupindu iliyopo Chumbuni mjini Unguja
na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa kambini hapo na baadae kupata maelezo kutoka
kwa uongozi wa Wizara ya Afya ambapo kwa upande wake Dk. Shein aliendelea
kusisitiza suala zima la usafi wa maji yanayotumiwa na wananchi sambamba na
kuzingatia usafi wa mazingira.
Dk.
Ramadhan Mikidadi ambae ni mkuu wa kambi hiyo, alimueleza Dk. Shein kuwa tayari
wagonjwa wengi wamefikishwa katika hospitali za Unguja na Pemba tokea kuanza
kipindupindu mnamo mwezi Septemba mwaka jana ambapo hivi sasa kuna wagonjwa
1788 wakiwemo 684 ambao hali zao si nzuri na tayari wagonjwa 40 wameshafariki.
0 comments:
Post a Comment