Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Visiwa vya Comoro, zina nafasi kubwa ya
kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Aidha,
nchi hizo zimeelezewa kwamba zinapaswa kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa
miaka mingi unaoambatana na udugu wa damu kati ya watu wa pande mbili
hizo.
Balozi
wa Comoro nchini Tanzania Dk. Ahamada Badaoul Mohamed, aliyemtembelea Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mhe. Ali Abeid Karume leo, amesema udugu wa
Comoro, Zanzibar na Tanzania kwa jumla, unapaswa kuongezewa nguvu.
Amesema
nchi hizo zinapaswa kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano, kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni.
Alieleza,
kwa kuwa nchi hizo ni visiwa, kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika
usafiri wa baharini ambao kwa muda mrefu umekabiliwa na uhaba wa miundombinu ya
uhakika.
Dk.
Badaoui amemueleza Waziri Karume kuwa, baada ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali
Mohamed Shein kutembelea visiwa vya Comoro miezi kadhaa iliyopita, nchi hizo
zilisaini mkataba wa ushirikiano unaofungua milango ya kuimarisha sekta za
uchumi kati yao.
Kupitia
makubaliano hayo, alisema nchi yake na Zanzibar ambazo zina vivutio vingi vya
utalii, zinalazimika kuvitumia kuongeza mapato yao kupitia safari za kitalii
miongoni mwao.
Kwa
upande wa sekta ya elimu, alifahamisha kuwa, wanafunzi wa Zanzibar
wanakaribishwa kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vya Comoro, kama wanafunzi
wa nchi yake wanavyoweza kuja kusoma katika vyuo mbalimbali vilivyoko hapa
nchini.
“Udugu
wetu wa damu na ushirikiano wa miaka mingi, ni mambo yanayotuunganisha na
lazima sote kwa pamoja tutafute njia za kuuimarisha na kuudumisha,”
alifahamisha.
Aidha
alisema Zanzibar na Comoro zinafanana kwa mengi, ikiwemo dini na tamaduni zake,
na kwamba nchi yake inaangalia uwezekano wa kuleta wanafunzi wake hapa nchini
kwa ajili ya kujifunza muziki hasa wa taarab.
Kwa
upande wake, Waziri Karume alieleza kufarijika na ujio wa Balozi huyo, na
kumtaka ajisikie yuko nyumbani kutokana na muingliano wa watu wa pande mbili
hizo.
Waziri
Karume amesema, hatua ya Zanzibar kununua meli mpya ya MV Mapinduzi II, ni
mwanzo mzuri wa kurejesha safari za kibiashara na za kutembeleana kati ya watu
wa nchi hizo.
Alisema
Zanzibar imekumbwa na misukusuko kadhaa ya ajali za baharini, lakini sasa hilo
litabaki kuwa historia, kwani MV Mapinduzi II ina uwezo mkubwa kuhimili
vishindo vya safari kutokana na muundo wake wa kisasa.
Balozi
Karume alieleza kuwa mafungamano kati ya wananchi wa Zanzibar na Comoro kwa
upande wa dini, tamaduni na ndoa, ni daraja muhimu la kuimarisha uhusiano wao
uliodumu kwa miaka mingi.
Maelezo Zanzibar-21/04/2016
0 comments:
Post a Comment