Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Aprili, 2016 amefungua rasmi Daraja la
Kigamboni linalounganisha usafiri wa barabara kati Kigamboni na Kurasini
Jiji la Dar es salaam na amependekeza Daraja hilo liitwe Daraja la
Nyerere (Nyerere Bridge).
Sherehe za ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la
kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati zimefanyika kando ya daraja hilo
upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali wakiwemo
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu
Youqing, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhandisi Edwin
Ngonyani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde, Wabunge na Mameya wa Jiji
na Dar es salaam.
Ujenzi wa daraja hilo umehusisha nguzo mbili
za pembezoni na mihimili miwili inayoshikilia nyaya 36, na daraja zima
lina urefu wa meta 680, upana wa mita 32, njia sita za magari, njia mbili za
watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5.
Daraja hilo limejengwa kwa fedha za ndani na
kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 254.12 ambapo kati ya fedha hizo
asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), na asilimia
40 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kujengwa kwa Daraja hili kutaondoa kero ya
msongamano wa magari na usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na wakazi wa
katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao walilazimika kutumia kivuko (Ferry) ili
kukatiza eneo la mkondo wa bahari ya Hindi ama kutumia barabara ya
kuzunguka kupitia Kongowe lenye urefu wa kilometa 52.
Daraja hilo limefanyiwa majaribio kwa kutumia
Malori 44 yenye uzito wa tani 30 na limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla
ya tani 1,320 na hivyo linatarajiwa kusaidia usafirishaji wa mizigo ya
kutoka na kuingia katika bandari ya Dar es salaam.
Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza vyombo
husika vianze mchakato wa daraja hilo kupewa jina la "Daraja la
Nyerere" (Nyerere Bridge) ikiwa ni kuuenzi mchango mkubwa wa Hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefanya kazi kubwa ya
kuijenga Tanzania.
Aidha , Rais Magufuli amewapongeza wadau wote
waliohusika kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo likiwemo Shirika la Hifadhi ya
Jamii (NSSF), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na wakandalasi
kutoka China, na ametaka watanzania wajivunie daraja hilo kubwa na
lililojenga heshima kubwa kwa nchi.
Pia Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa
vyombo vya habari vya Tanzania
kuitangaza vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza kazi nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.
kuitangaza vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza kazi nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli
amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe na
kuagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma
zinazomkabili za kusaini mikataba iliyosababisha serikali kupoteza mapato.
Dkt.Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati
akitoa hotuba ya ufunguzi wa
daraja la Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda kumueleza kuwa amebaini upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe kusaini mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kwa kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa tozo za uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.
daraja la Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda kumueleza kuwa amebaini upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe kusaini mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kwa kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa tozo za uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
Dar es salaam
19 Aprili, 2016
0 comments:
Post a Comment