March 14, 2016

Wazanzibari wametakiwa kutokubali kuwaachia watu wasioijua lugha ya Kiswahili kuiharibu, na badala yake wasimame kidete kuilinda na kuiendeleza.
Akizungumza na washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Zanzibar yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Vuga, Rais mstaafu wa Tanzania Mhe. Ali Hassan Mwinyi, alisema wakati umefika kuwaongoza wanaofanya makosa ya kimaandishi na matamshi katika lugha hiyo.
Alifahamisha kuwa, katika siku za karibuni, kumezuka mtindo wa kubadilisha maneno ya Kiswahili kutoka kwenye uasili wake na kuyapopotoa.
Alitoa mfano wa baadhi ya watu kutamka nane pahala panapostahili neno ‘manane, vinane au wanane’, mathalan kusema au kuandika ‘watu nane’, matamishi ambayo si sahihi.
“Siku hizi imekuwa fasheni (mtindo) kuyabadilisha maneno ovyo na hili hufanywa zaidi na watu wasiokifahamu Kiswahili, lakini wenye lugha yao wapo na hawachukui hatua yoyote kuwarekebisha,” alifafanua.
Mzee Mwinyi alisema visiwa vya Zanzibar ndio shina la Kiswahili hivyo wananchi wake hawana budi kukitetea na kuhakikisha kinashika nafasi yake kwa kuwaongoza wale wanaofanya makosa na kuwaelekeza katika usahihi.
“Tusivunjike moyo, tuwafahamishe taratibu na hatimaye watafahamu kwani papo kwa papo kamba hukata jiwe,” alisisitiza mwalimu huyo mkereketwa wa lugha ya Kiswahili.
Katika hatua nyengine, aliziomba serikali zote mbili za Zanzibar na Tanzania, kuwapatia mikopo wanafunzi wote wanaotaka kusoma Kiswahili katika vyuo vya elimu ya juu, kwani wao ndio watakaokuwa watendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki ambayo makao makuu yake yameamuliwa kuwa Zanzibar.
Pamoja na kuupongeza uongozi wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kwa uamuzi wake wa busara kuchagua siku ya kuitukuza lugha hiyo, Mzee Mwinyi pia amewahimiza wananchi mbalimbali kununua vitabu na majarida mengine yanayochapishwa na Baraza hilo, yakiwemo makamusi ya lahaja za Kizanzibari ili kukisoma na kukijua vyema Kiswahili.
Aidha, aliziomba serikali zote mbili kuzijengea uwezo taasisi zote zinazofanya kazi ya kukiendeleza Kiswahili ili kiweze kusambaa kwa haraka kote ulimwenguni.
Mapema, Katibu Mtendaji wa BAKIZA Mwanahija Ali Juma, alisema baraza hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali za upotoshwaji wa Kiswahili unaofanywa kwa kisingizio cha maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Alisema miongoni mwa jitihada za BAKIZA katika kuiendeleza lugha hiyo, ni kufanya utafiti wa lahaja kwa ajili ya kuandika makamusi, ingawa kazi ya kuchapisha miswada hukwamishwa na ukosefu wa fedha.
Katika hafla hiyo iliyopambwa na shairi na igizo yaliyokuwa na maudhui ya kukiimarisha Kiswahili na lahaja zake, mgeni rasmi Mzee Ali Hassan Mwinyi alizindua jarida lililopewa jina la Jahazi, pamoja na kukabidhi zawadi kwa mshindi wa kuandika tamthilia pamoja na washiriki wengine wa shindano hilo.
Huu ni mwaka wa tisa tangu kuasisiwa kwa siku ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili Zanzibar mwaka 2007, na ujumbe wa mwaka huu ni ‘Sayansi na Teknolojia zitumike kuendeleza Kiswahili’.  



:Maelezo Zanzibar


0 comments:

Post a Comment