STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS
RELEASE
Zanzibar 10 Machi, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya
Vietnam Mheshimiwa Truong Tang Sang ambaye yuko nchini kwa ziara rasmi ya
kiserikali ya siku nne kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Katika mazungumzo hayo rasmi yaliyofayika jana
Ikulu jijini Dar es salaam, Dk. Shein amesema uhusiano mzuri wa kisiasa na
kidiplomasia kati ya Tanzania na Vietman unatoa fursa ya kipekee kwa nchi mbili
hizo kuimarisha ushirikiano katika maeneo mengine ambayo
yataharakisha maendeleo na kujenga ustawi wa wananchi wa pande mbili hizo.
Aliongeza kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla
zina mengi ya kujifunza kutoka Vietnam hivyo alihimiza ushirikiano zaidi kati
ya Zanzibar na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi na
ufugaji wa samaki, utalii,biashara na uwezeshaji wananchi vijijini.
Dk. Shein na Rais
Truong walikubaliana kuwa mapendekezo ya miradi miwili mikubwa katika kilimo na
uvuvi kati ya Zanzibar na Vietnam ambayo ni matokeo ya ziara ya Dk. Shein
aliyoifanya nchini Vietnam mwaka 2012 utekelezaji wake ushirikishe pia sekta
binafsi za nchi hizo.
Alieleza kuwa mapendekezo ya miradi hiyo ni
hatua moja muhimu kuelekea ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na maendeleo
kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Alifafanua kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ni kuhakikisha usalama wa chakula na kwa kuwa chakula kikuu cha
wananchi wa Zanzibar ni mchele, mkakati wa serikali ni kuimarisha kilimo cha
mpunga hivyo ingependa kutumia uzoefu na maarifa kutoka
Vietnam kufanikisha azma hiyo.
Dk. Shein alimweleza Rais Truong kuwa Zanzibar
ina fursa nyingi za uwekezaji na kwamba milango iko wazi kwa wawekezaji kutoka
Vietnam kuwekeza katika sekta mbali mbali zikiwemo kilimo, uvuvi wa bahari kuu
pamoja na utalii.
Katika mazungumzo hayo, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimueleza Rais Truong kuwa amefurahishwa na
ziara yake nchini Tanzania ambapo imewawezesha kukutana kwa mara ya pili baada
ya ziara yake aliyoifanya nchini Vietnam mwaka 2012.
Dk. Shein alibainisha kuwa Vietnam na Tanzania
ni marafiki kwa kweli na daima serikali na wananchi wa nchi hizo wameonesha kwa
vitendo utayari wao wa kuzidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao.
Kwa upande wake Rais wa Vietnam Mheshimiwa
Truong alieleza kuwa ziara yake nchini Tanzania imekuwa ya mafanikio makubwa na
anaamini kuwa imefungua ukurasa mpya katika kuimarisha uhusiano wa nchi yake na
Tanzania.
Alibanisha kuwa mazungumzo yake na Rais
Magufuli pamoja na makubaliano yaliyofikiwa yataongeza kasi ya ushirikiano
katika maeneo mbali mbali ya ushirikiano ikiwemo biashara.
Rais Truong alisema kuwa iko haja ya kukuza
kiwango cha biashara kati ya nchi yake na Tanzania na kuongeza kuwa anatambua
fursa nyingi za uwekezaji zilizopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kwamba
mafanikio ya baadhi ya wawekezaji waliowekeza nchini yataongeza hamasa ya
wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza Tanzania.
Nchi yake alisema iko tayari kushirikiana na
Zanzibar katika sekta za kilimo, Utalii, uvuvi na katika maeneo mengine na
kusisitiza Vietnam ingependa kuona ushirikiano madhubuti zaidi na Zanzibar.
Rais Troung alipendekeza kuwepo uhusiano kati
ya miji ya Zanzibar na Vietnam pendekezo ambalo lilikubaliwa na Dk.
Shein.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alifuatana na
Mawaziri na Makatibu wa wakuu wa Wizara za Kilimo, Afya, Biashara, Uvuvi na Mifugo
pamoja na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Mheshimiwa Dk.
Mwinyihaji Makame.
0 comments:
Post a Comment