February 27, 2016

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na sekta binafsi za kuwasaidia wananchi  miradi mbali mbali ya kimaendeleo inayofanywa kwa nia ya kupunguza umaskini katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Afya Zanzibar , Halma Maulid Salim wakati akikabidhiwa vifaa vya Hospitali na  Shirika la misaada ya kijamii la Helping Hand kutoka Marekani, huko katika skuli ya Muzdalifah Islamic Charitable Organization(MICO) Zanzibar iliopo Mitondooni Kisauni.
Ameeleza kuwa taasisi binafsi zimeweza kuisaidia serikali katika kufanya miradi na kuomba misaada mbali mbali ya maendeleo ili iwanufaishe wananchi wengi hasa wanaoishi vijiji.
Bi, Halima amesema vifaa hivyo vitasaidia utoaji wa huduma bora za kiafya nchini katika Vituo vya afya vitakavyonufaika na msaada huo ili  kuhakikisha kila mwananchi anapata huduza za uhakika.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vigari vya watu wenye ulemavu 6, vitanda vya hospitalini 6, kitanda cha wagonjwa mahututi  1, vitanda vya dharura 2, mipira ya haja ndogo 2000, visaidizi vya kutembelea kwa watu waliopata ajali 40, miguu bandia ya watu wenye ulemavu pamoja na viatu vyote vikiwa na thamani ya Dola za kimarekani 345,320.
Akikabidhi vifaa hivyo Mwakilishi kutoka Helping Hand kutoka Marekani, Mohammed Habibu amesema msaada huo ni miongoni mwa fursa zinazotolewa na shirika hilo kwa nchi mbali mbali duniani zinazokabiliwa na upungufu wa vifaa vya kisasa katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Ameeleza kuwa kutokana na sifa ya Zanzibar na watu wake shirika hilo litaendelea kuweka mipango endelevu ya kuhakikisha watapata misaada katika sekta mbali mbali kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Muzdalifah Islamic Charitable Organization(MICO), Farouk Hamad amesema vifaa hivyo ni miongoni mwa matunda ya miradi ya kusaidia jamii ya Zanzibar inayoombwa  na jumuiya hiyo kwa wahisani mbalimbali.

Ameeleza kuwa licha ya jumuiya hiyo kubuni miradi mbali mbali ya kuisaidia jamii katika nyanja za kiuchumi na kijamii bado wanawabiliwa na changamoto ya ukosefu wa dawa katika kituo cha afya kinachomilikiwa na jumuiya hiyo, pamoja na upungufu wa wafanyakazi kutokana na ufinyu wa vyanzo vya mapato.

0 comments:

Post a Comment