STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.2.2016
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisistiza haja ya
kuimarishwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Kuwait hasa
katika kushajihisha sekta ya uwekezaji.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na
Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kuwait Mhe. Dk. Mahadhi Juma Maalim ambaye anakuwa Balozi
wa mwanzo katika Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Kuwait.
Katika mazungumzo
hayo Dk. Shein alimueleza Balozi huyo Mteule kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar
inajivunia uhusiano na ushirikiano uliopo hivyo iwapo sekta ya uwekezaji
itapewa kipaumbele baina ya nchi mbili hizo mafanikio makubwa yanaweza
kupatikana.
Aidha, Dk. Shein
alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Kuwait katika kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika
kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na hatua kubwa zilizofikiwa katika kuimarisha
sekta ya utalii hapa nchini ipo haja kwa nchi hiyo kuendeleza uhusiano na
ushirikiano katika sekta hiyo muhimu ambayo inaipatia fedha nyingi za kigeni
Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Alieleza kuwa
Tanzania ni nchi ambayo imejaaliwa kuwa na vivutio mbali mbali vya utalii
zikiwemo mbuga za wanyama kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na fukwe zenye
kuvutia kwa upande wa Zanzibar ambavyo vimeweza kuwavutia wageni wengi kuja
kuitembelea Tanzania.
Pia, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Mahadhi azma ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuimarisha sekta ya ajira kwa vijana na kueleza haja kwa nchi
hiyo kuimarisha mashirikiano katika sekta hiyo.
Sambamba na
hayo, Dk. Shein alimtakia heri na fanaka kubwa Balozi Mahadhi katika utendaji
wake wa kazi kwenye Ubalozi huo mpya wa Tanzania nchini Kuwait na kueleza kuwa
kwa vile anatambua utendaji wake wa kazi ana matumaini makubwa kwa balozi huyo
na Ubalozi huo kuweza kupata mafanikio na kuendelea kuijengea hadhi kubwa
Tanzania Kitaifa na Kimataifa.
Nae Balozi huyo Mteule
wa Tanzania nchini Kuwait kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kupata uteuzi huo mpya ambapo
kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Dk. Mahadhi
alimuhakikikishia Dk. Shein kuwa katika wadhifa wake huo mpya juhudi za
makusudi atazichukua kwa mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha uhusiano na
ushirikiano uliopo kati ya Kuwait na Tanzania unaimarishwa zaidi sambamba na
kuimarisha maslahi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment