February 10, 2016

Jeshi la polisi Zanzibar limewatahadharisha mtu au kikundi cha watu kinachotoa vitisho kwa wananchi hata kushindwa kufanya shuguli zao za  kawaida.
Naibu Mkuregenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Zanzibar Salum Msangi amesema kumejitokeza vitendo vya kusambazwa vipeperushi vyenye vitisho, kikundi kinachotesa watu (mazombi) na kuwekwa alama za X kwenye baadhi ya nyumba hasa Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Zanzibar amemtaka yeyote anayehusika na utoaji wa vitisho hivyo kuacha mara moja kabla ya jeshi la polisi kuchukua hatua kali dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
 “ kuna vikaratasi vimesambazwa vyenye ujumbe usemao ipo siku itakuwa kweli  ‘One Day Yes’ changine ni  “Kutangazwa uchaguzi siyo kufanyika uchaguzi.”
Msangi amefahamisha kuwa juhudi za kuubini mtandao huo zinafanywa kwa ushirikiano na jeshi hilo na taasisi nyengine za ulinzi za kitaifa na kimataifa ili kukomesha tabia hiyo.
Akizungumzia kuhusu kikundi cha mazombi kinachowapiga raia huku wakiwa wamejifunika vitambaa au soksi usoni amefahamisha kuwa  jeshi la polisi  halilitambui kundi hilo kwa vile wanaofanyiwa vitendo hivyo hawatoi taarifa kwa jeshi hilo ili kuweza kufanya uchunguzi wa kuwabaini.
Amewataka madaktari kuacha kuwahudumia watu wanaokwenda hospitali baada ya kupigwa na kikundi hicho bila ya kuwa na fomu ya matibabu (PF3) kwani ni kinyume ch sheria.
“Kwa mujibu wa taratibu zilizopo mtu yeyote anayefanyiwa kitendo cha kihalifu anapaswa kutoa taarifa kituo cha polisi ili uchunguzi au upelelezi ufanyike kubaini wahalifu hao na iwapo tutabaini daktari ametoa tiba kwa watu hao bila fomu ya PF3 itamchukulia hatua", amesema Msangi.
Aidha  amezungumzia juu ya baadhi ya nyumba kuwekwa alama ya X hasa Pemba amesema polisi imeshabaini madhumuni na nia ya vitendo hivyo na baadhi ya walihusika kufanya hivyo wameshatuambiliwa na wanakamilisha ushahidi ili kuwachukulia hatau wahusika.

Jeshi hilo la polisi limewahakikisha wananchi kuwa uchaguzi wa marejeo wa Marchi 20 2016 utafanyika kwa njia ya  amani na utulivu  na haitosita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakaefanya vurugu au kitendo kinachoashiria uvunjifu wa amani.

0 comments:

Post a Comment