Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe
Magufuli kwa kutimiza ahadi yake ya kuipatia Mahakama kiasi cha shilingi
Bilioni 12.3 alizoahidi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4,
2016 jijini Dar es salaam.
Amesema Fedha hizo zitatumika katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu
ya Mahakama na ujenzi wa Mahakama mpya katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa shukrani hizo leo jijini Dar es salaam
Mhe.Othman amesema kuwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 Mahakama imepata
asilimia 100 ya fedha zote za Maendeleo zilizokasimiwa na Bunge kwenye Bajeti
yake ya mwaka 2015/2016.
Amesema kupatikana kwa fedha hizo ambazo
ni za Maendeleo kutasaidia kufufua miradi ya ujenzi iliyosimama, kufufua
Mahakama ambazo zilikua hazifanyi kazi kwa sababu ya uchakavu na kuipatia
Mahakama fursa zaidi ya kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwasogezea huduma
za Haki karibu katika maeneo wanayoishi.
Mhe.Othman ameeleza kuwa kwa kipindi cha
bajeti za miaka 3 mfululizo kuanzia mwaka 2012 /2013 hadi 2014/2015 Mahakama
ilikua ikipokea fedha pungufu ya kiasi kilichopangwa katika Bajeti hali
iliyochangia kuzorota kwa shughuli za Mahakama.
” Kwa mara ya kwanza Mahakama tumepata
asilimia 100 ya Bajeti yetu ya mwaka 2015/2016 kutoaka Serikalini, mwaka
2012/2013 tulipata shilingi bilioni 26.9 ikiwa ni pungufu ya bajeti yetu kwa
asilimia 78, mwaka 2013/2014 tukapata Bilioni 42.7 pungufu kwa asilimia 82 na
mwaka 2014/2015 tulipewa shilingi bilioni 41.5 ambayo ni pungufu kwa
asilimia 92 “
Akizungumzia miradi ya ujenzi wa majengo mapya
ya Mahakama amesema kuwa tayari Mahakama ina michoro ya ramani za majengo
yatakayojengwa katika maeneo mbalimbali ambayo hayakuwa na huduma hiyo ikiwemo
mikoa 12 kati ya 25 ambayo haina Mahakama Kuu, wilaya 22 kati ya 133 ambazo
hazina Mahakama za Wilaya pamoja na kuongeza Mahakama za Mwanzo ambazo ziko 976
kufikia kata zote 3,957.
Kuhusu Mradi wa ujenzi wa jengo la
Makao Makuu ya Mahakama utakaofanyika katika uwanja wa Chimala jijini Dar es
salaam amesema utahusisha maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za
Kimahakama na kuongeza kuwa Mahakama itajenga jengo lenye viwango
kwa kuwatumia Wakandarasi na wataalam wa kitanzania watakaojenga
Mahakama nzuri na yenye viwango kwa gharama nafuu.
“Mahakama tutatoa kipaumbele kwa wataalam wetu
wa ndani ili waweze kutujengea Mahakama zetu, tunalenga kuwafikishia huduma
zetu katika maeneo wanayoishi tunao mfano mzuri wa Mahakama ya mwanzo ya
Dumila iliyoko Morogoro, Mahakama hii imejengwa kijijini ni ya kisasa” Amesisitiza
Mhe.Othman.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria
Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na
Mahakama ya Tanzania ili kuwezesha ufanisi wa shughuli zake kwa kuhakikisha
kuwa kiwango cha fedha za Bajeti kinachopitishwa kwa ajili ya kuhudumia
shughuli za Mahakama kinafika kwa wakati.
Akizungumzia kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya
Mafisadi, amesema uanzishwaji wake uko katika hatua nzuri na wakati ukifika
wananchi watataarifiwa kama ilivyoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kuungwa mkono na Mahakama ya Tanzania.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango, akizungumzia fedha za Maendeleo zilizotolewa na Mhe.
Rais amesema kuwa lengo la ahadi ya Rais kwa Mahakama ilikua ni kuhakikisha
Haki inapatikana kwa wananchi kwa Wakati na miongoni mwa vitu vilivyokua
vikichelewesha haki kwa watanzania walio na mashauri Mahakamani ni ukosefu wa
fedha na uchakavu wa miundombinu.
Amesema Serikali inaendelea kujenga uwezo wa
kifedha ili kuimarisha huduma katika mihimili yote ikiwemo Bunge na Mahakama
huku msisitizo ukiwekwa katika kukusanya mapato ya ndani.
“Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) tuna dhamira ya dhati ya kukusanya mapato ya ndani ili kujenga
uwezo wa Serikali tutawabana wote waliokuwa wanakwepa kulipa kodi na hili
tutalisimamia kikamilifu”
Amesema utoaji wa Haki ni moja ya ukuzaji wa
maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa Mahakama ya Tanzania inafanya kazi nzuri
pamoja na ufinyu wa bajeti yake.
0 comments:
Post a Comment