February 15, 2016




Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Watoto na Wazee   Ummy Mwalimu amewasimamisha wakurugenzi toka Bohari ya Dawa ya Taifa(MSD) kwa ubadhilifu wa fedha takribani Shillingi Billion 1.5.
Wakurugenzi hao wa  Bohari ya dawa MSD ni  pamoja na Mkurugenzi wa kanda huduma kwa wateja Cosmas Mwaifwani, Mkurugenzi wa fedha Joseph Tesha, Mkurugenzi wa ugavi Misanga Muja na Mkurugenzi wa manunuzi Henry Mchunga.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto baada ya kupokea  vifaa toka Bohari Kuu ya Dawa ya Taifa (MSD) amesema amepata taarifa ya uchunguzi ofisini kwake ya ubadhilifu wa kiasi hicho cha fedha na kuamua kuwasimamisha wakurugenzi wanne kupisha uchunguzi.
Amewataja viongozi hao ni Joseph Tesha Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Misanga Muja Mkurugenzi wa Ugavi, Heri Mchunga Mkurugenzi wa Manunuzi na Cosmas Mwaifani Mkurugenzi Kanda na Huduma kwa Wateja na amewataka Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari ya Dawa ya Taifa kuwaandikia barua mara moja ya kuwasimamisha kazi.
“ Nimeletewa taarifa ofisini kwangu na nimeamua kuchukua fursa hii kuwaambia na hili pia kwamba nimewasimamisha wakurugenzi wanne toka Bohari ya Kuu Dawa ya Taifa kwa ubadhilifu wa fedha na nisingeweza kusubiri nitumbuliwe mimi jipu na Mhe. Rais kwa hiyo  nimeamua kuwachukulia hatua kwa kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi”
“ Hizi ni zama za kufanya kazi na kuwajibika sasa inabidi tuwajibike kwa kufanya kazi na hatutowavumilia watendaji watakaoenda kinyume na utaratibu katika ofisi yoyote ile katika sekta ya afya na tutawachukulia hatua kwani tunataka uwajibikaji ili kuiendeleza sekta ya afya ambayo  ni muhimu sana kwa kila mwanadamu” amesema Ummy.
Katika kuboresha sekta ya afya nchini Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee imejipanga kufanya kazi  kwa taratibu na misingi iliyopo ili kuhakikisha inapeleka mbele gurudumu la maendeleo ya hasa katika sekta ya afya kwa ujumla.
 

0 comments:

Post a Comment