December 28, 2015

Hali mbaya na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya kupata maeneo ya ujenzi umekithiri kwa kiwango kikubwa na kutishia usalama wa  mazingira ya visiwa vya Zanzibar.
Miti iliyoathirika zaidi ni minazi na inakisiwa zaidi ya milioni 4 imekatwa maeneo mbalimbali ya mkoa wa mjini magharibi katika  ardhi za mshamba walizopatiwa wananchi na serikali kuyaendeleza.
Mkurugenzi wa idara ya misitu na maliasili zisizorejesheka Zanzibar Sheha Idrissa Hamdan amesema wilaya ya magharibi A na B ndio zilizoathirika zaidi kutokana na kasi kubwa ya ujenzi wa makaazi na  watu wanajenga bila ya kufuata taratibu zilizowekwa serikali.
“ Tumebaini minazi milioni 9 kati ya milioni 13 imeshakatwa katika kipindi cha miaka 10 watu wanajiamulia tu pasi na kuwaarifu idara inayoshughulika na ardhi halmashauri ” amefahamisha.
Ameeleza kwa suala  hilo halikubaliki kufumbiwa macho hatua za lazima zinapaswa kuchukuliwa ili kunusuru zao hilo lisipotee kabisa.
Mkurugenzi Hamdani amefahamisha kuwa athari za ukataji wa minazi kiholela zimeshaanza kuonekana ikiwemo Zanzibar kuanza kutegemea nazi kwa ajili ya matumizi kutoka Tanzania bara wakati ilikuwa miongoni mwa vinara wa kusafirisha  zao hilo pamoja na mafuta na mbata nje ya nchi.
Akizungumzia juhudi wanazochukuwa amesema wamepitisha sheria namba 10 ya kulinda misitu na hivi karibuni Serikali imetoa sheria mpya ya kudhibiti msumeno wa moto na Disemba 7 2015 ilikuwa tarehe ya mwisho ya watu wanayoimiliki kuirejesha lakini inaendelea kutumika kwa siri kukata miti.
Hamdani amesisitiza kuendelea kuelimisha na kuhamasisha utunzaji wa misitu kwa vile bado wapo wahalifu wachache wanakiuka hayo ili kuhakikisha matumizi ya rasilimali yanaendana na utaratibu uliowekwa.
Hata hivyo amesema zanzibar haijachelewa kuchukuwa hatau hizo lakini ni vyema kuwepo na ushirikiano kati ya taasisi mbalibali zikiwemo za wilaya, halamashauri na vyombo vya ulinzi ili asilimia 40 ya eneo la  Zanzibar lenye msitu kuendelea kudumu kwa faida ya nchi.

0 comments:

Post a Comment