December 13, 2015


Uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja umetoa muda wa wiki mbili kwa hoteli ya  Palumbo reef Beach Resort ya Uroa kuondoa mawe waliyoyaweka katika maeneo ya ufukwe iliyopo karibu na hoteli hiyo.
Pia umekataza pia uchotaji  mchanga katika maeneo ya fukwe za bahari za kigaeni Makunduchi na ukataji  wa miti ya  mikoko  katika eneo la  Bwejuu banja.
Mkuu wa mkoa huo Dkt Idrissa Muslim Hijja amesema vitendo hivyo vinahatarisha kupotea rasilimali hizo zisizorejesheka pamoja na kupoteza haiba ya maeneo ya fukwe ambayo ni moja ya kivutio kwa utalii wa Zanzibar
Akitoa agizo la kwa hoteli ya  Palumboreef Beach Resort amesema mawe hayo yameziba njia na kusababishia kero kubwa kwa wanakijiji cha uroa kupita njia hiyo wanayoitumia kufanya shughuli zao mbali mbali za kijamii ikiwemo ya uvuvi na ukulimaji mwani.
Dkt Idrissa  amefahamisha kuwa hoteli hiyo imekiuka  taratibu za sheria kutokana na muwekazaji huyo kutokuwa na kibali chochote  kinachomruhusu kuziba njia hiyo jambo linaloweza kusababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo ya fukwe za bahari.
Aidha  amesisitiza kwa wawekezaji  kuacha kujichukulia maamuzi yao  kinyume na taratibu za  zilizowekwa na serikali  na badala yake ni vyema kufuata sheria pamoja na kujenga uhusiano mzuri  na wanavijiji ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima.
 Nae Mkuu wa wilaya ya kusini unguja Khamis Jabir Makame  akizungumzia marufuku ya  uchotaji wa mchanga katika maeneo ya fukwe za bahari  na ukataji  wa miti ya  mikoko amesema serikali  haitomvumilia mwananchi yoyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo kwani  vinaleta athari kubwa za uharibifu wa mazingira.
ameliagiza jeshi la polisi kwa kushirikiana na maofisa mazingira na misitu kuhakikisha wanalishughulikia ipasavyo suala hilo ili kukomesha vitendo hivyo.
Afisa mazingira wilayani humo Ramadhani Haji Ameri amesema  pamoja na hatua zinazochukuliwa za kuelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira baharini bado wanapuuza suala hilo na kuendeleza kwa kasi vitendo hivyohali inayorudisha nyuma juhudi za serikali katika kulinda rasilimali za taifa.

0 comments:

Post a Comment