December 27, 2015

Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar kimewataka wanachama wake kujiweka tayari na kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi wa  marudio mara tarehe  itakapotangazwa.
Wakati CCM ikitoa kauli hiyo Chama cha Wananchi CUF Zanzibar kimesema hakipo tayari kupokea maazimio ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa Uchaguzi Mkuu kama yatakuwa yanakwenda kinyume na maamuzi waliofanya wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 Mwaka huu uliofutwa.
Kauli ya ccm imetolewa katika taarifa kwa waandihsi wa habari kuhusu kuhusu kikao cha siku moja cha kamati maalum ya NEC Zanzibar kilichofanyika  afisi kuu ya ccm Kisiwandui mjini Unguja iliyosainiwa na Katibu wa Kamati Maalum ya itikadi na Uenezi Waride Bakari Jabu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo imewataka wafuasi wake kujitayarisha ili kukiletea ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kuanzia Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wakati utakapowadia.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kikao hicho kilichofanyika leo Jumapili kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Ali Mohamed Shein ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kimeridhia pia majadiliano yanayoendelea kuhusu hali ya Kisiasa Zanzibar yanayoshirikisha Viongozi kadhaa.
Viongozi hao ni pamoja na Marais Wastaafu wa Zanzibar Ali Hassan Mwinyi, Mhe, Dkt. Salmin Amour Juma na Amani Abeid Karume, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.  
Aidha kimempongeza  Dkt. John  Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  baada ya kushinda  katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na  Samia Suluhu Hassan, kuwa Makamu wa Tanzania.



0 comments:

Post a Comment