December 29, 2015

Chama cha Wananchi CUF kimewataka Wazanzibari kusubiri taarifa rasmi ya matokeo ya mazungumzo yanayowahusisha viongozi wakuu wa kisiasa yanayofanyika Ikulu Zanzibar ambayo yapo katika hatua za mwisho kumalizika.
Chama hicho pia kimetaka pia kupewa nafasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli anaendelea na juhudi katika ngazi za juu kabisa za kuhimiza kupatikana ufumbuzi wa haraka wa mgogoro wa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
Taarifa ya kaimu Mkurugenzi wa habari na mawasiliano na umma CUF Ismail Jussa katika kikao na waandishi wa habari mjini Zanzibar imewahakikishia Wazanzibari kuwa haitotetereka na itasimamia kwa dhati maamuzi yao waliyoyafanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu huo.
Aidha imewapongeza wananchi kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa na kuendelea kutunza amani na utulivu wakati wakisubiri matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya tarehe 25 Oktoba, 2015  inayoashiria ujenzi wa Zanzibar Mpya.

Kauli hiyo ya CUF imetolewa baada ya taarifa ya hivi karibuni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  katika kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana Zanzibar juzi, tarehe 27 Desemba, 2015 iliyowataka wanachama wake kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa marejeo mara tarehe itakapotangazwa.

0 comments:

Post a Comment