Wagombea wa urais Zanzibar wametakiwa
kuwa na moyo wa subira na kutoa nafasi kwa mazungumzo yanayoendelea ya kusaka
muafaka wa mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar baada ya matokeo kufutwa Oktoba 28,
mwaka huu.
Wito huo ulitolewa na mgombea wa
urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Tadea, Juma Ali Khatib, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mazungumzo ya kusaka muafaka
yanayofanywa na viongozi wa kitaifa wakiwamo marais wastaafu visiwani humo.
Khatibu alisema mazungumzo
yanayofanyika yana umuhimu mkubwa katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa
uchaguzi kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
“Zanzibar inapita katika wakati mgumu
wa kisiasa na kiuchumi kutokana na hali ya maisha ya wananchi kubadilika tangu
kuibuka kwa mgogoro wa uchaguzi Oktoba 28 mwaka huu.”
Alisema hali ya biashara Zanzibar
imetetereka na kusababisha mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa na kuwataka wananchi
pamoja na kuwapo hali hiyo kuendeleza kudumisha amani na umoja wa kitaifa
wakati viongozi wa kitaifa wakitafuta muafaka wa mgogoro huo.
“Sie kama wagombea ni muhimu tuwe na
moyo wa subira, tuyape nafasi mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa
Zanzibar,” alisema Khatibu ambaye alikuwa akiwania urais wa Zanzibar kwa mara
ya tatu.
Hata hivyo, alikosoa akisema
haikuwa sahihi mazungumzo ya kusaka muafaka wa uchaguzi wa Zanzibar
kushirikisha wagombea wawili, Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif
Sharif Hamad wa Cuf kati ya 14 waliopitishwa na Zec kuwania wadhifa huo.
Alisema wagombea
wote walikuwa na sifa na haki sawa, hivyo haikuwa sahihi kutengwa katika meza
ya mazungumzo baada ya Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, kufuta
matokeo ya uchaguzi.
:Nipashe
0 comments:
Post a Comment