Serikali imepiga marufuku uuzaji na ununuzi wa karafuu usio
rasmi (vikombe) kuepusha wizi wa zao hilo mashambani na ukataji wa mikarafuu unaofanywa
na baadhi ya watu kutokana na kuzoeleka kwa biashara hiyo.
Wakizungumza katika nyakati tofauti Wakuu wa Wilaya za Unguja na
Pemba wamesema hakuna ruhusa kwa mtu yoyote kuuza au kununua karafuu mbichi au
kavu na atakaebainika kujihusisha na biashara hiyo atashughulikiwa ipasavyo.
Wamebainisha kuwa Serikali haiwezi kuvumilia makosa hayo kwa
sababu wanaofanya uhalifu huo hawana imani na Serikali haina imani nao hivyo
kwa watakaokamatwa watachukuliwa hatua kwa misingi ya kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Haji Makungu Mgongo amesema
karafuu ni zao la uchumi wa Taifa hivyo Wilaya hiyo haitokuwa tayari kuona baadhi ya watu
wakihujumu kwa wizi hasa kukata mkarafuu kwa tamaa ya kupata maslahi ya muda
mfupi.
Mwanasheria wa Shirika la ZSTC Ali Hilal Vuai amesema kuiba
karafuu ama kukata mikarafuu kwa
matumizi mengine yoyote ni makosa kwa mujibu wa sheria namba 2 ya Maendeleo
ya Karafuu ya mwaka 2014.
Amesema sheria hiyo inakataza kuihujumu
mikarafuu kwa aina yoyote ile na atakaebainika kufanya vitendo hivyo anapaswa kupelekwa
katika vyombo vya sheria.
0 comments:
Post a Comment