STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana alikagua shughuli
mbalimbali za miradi ya uwekezaji katika maeneo huru ya Fumba nje kidogo ya mji
wa Zanzibar na kueleza kuridhishwa kwake na kasi ya uendelezaji wa
miradi aliyoitembelea.
“haya ndio maendeleo
tunayoyataka na hatuna budi kuyatangaza ili watu walijue eneo hili la Fumba
lenye mwelekeo mpya kabisa wa maendeleo ya kisasa” alisema Dk. Shein.
Katika ziara hiyo
alitembelea Mradi wa Maendeleo ya Mji wa Fumba (Fumba Uptown Living Project)
unaojumuisha ujenzi wa nyumba 500 za aina na ukubwa tofauti pamoja na huduma
nyingine za kijamii,ujenzi wa gati ndogo na mitambo ya ujenzi wa barabara.
Mradi huo unajengwa kwa
ushirikiano kati ya Serikali na Makampuni ya Bakhresa (Said Salum Bakhresa
Group of Companies).
Dk. Shein aliupongeza
uongozi wa Makampuni ya Bakhresa chini ya kiongozi wake Sheikh Said Bakhresa
kwa kuonesha mfano katika uwekezaji katika mradi huo mkubwa ambao sio tu
utaibadilisha kabisa haiba ya mji wa Fumba lakini kuipatia sifa zaidi Zanzibar.
Akitoa maelezo kwa
Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti wa Makampuni ya Bakhresa Sheikh Said Salum Bakhresa
alieleza kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo utakaogharimu zaidi dola za
kimarekani milioni100, utahusisha ujenzi wa nyumba 100 utakaoanza mwezi ujao.
Alifafanua kuwa katika
kurahisisha usafirishaji wa vifaa vya mradi huo, kampuni yake itajenga gati
ndogo ambayo itawezesha vifaa na mahitaji mengine ya mradi kwenda moja kwa moja
Fumba.
Hata hivyo aliongeza
kuwa baada ya mradi kukamilika bandari hiyo itaimarishwa ili itumike kwa
shughuli za kusafirishia abiria na mizigo kwa boti za kampuni yake na nyingine
kati bandari za Zanzibar na maeneo mengine ya Pwani ya Afrika Mashariki.
Mbali na nyumba sehemu
ya mji huo hasa sehemu ya kilomita 2 inayotazamana na bahari itajengwa sehemu
za kupumzikia wakaazi na wageni watakaotembelea eneo hilo, sehemu za burudani,
michezo ya watoto, mikahawa, maduka na michezo ya maji (water park).
Sheikh Said Bakhresa
alisema anaamini kuwa kuanza kwa ujenzi huo kutavutia wawekezaji wengi zaidi
kuja katika eneo hilo na kwamba hana shaka yeyote baada ya miaka michache ijayo
sehemu hiyo itakuwa mashuhuri kama sehemu nyingine maarufu duniani.
Katika maelezo yake
hayo, aliipongeza na kuishukuru Mamlaka ya Kuendeleza Vitega Uchumi Zanzibar
(ZIPA) kwa ushirikiano wao wa karibu na kuongea kuwa hivi sasa mamlaka hiyo
imepunguza urasimu na kuongeza ufanisi. Alizishukuru pia mamlaka nyingine kwa
ushirikiano wao ambao umewezesha mradi huo kuanza utekelezaji wake.
Awali akitoa maelezo kwa
Mkurugenzi Mkuu wa ZIPA Ngd. Salum Khamis Nassor alisema utaratibu
wa sasa maombi ya mradi yanapaswa kujibiwa ndani wiki mbili na ofisi yake
imekuwa ikiutekeleza utaratibu huo ipasavyo.
Kuhusu ujenzi wa
miundombinu ya barabara katika eneo hilo la uwekezaji la Fumba, Mkurugnezi Mkuu
huyo alibainisha kuwa barabara zenye urefu wa kilomita 12 zimo mbioni kujengwa
kuzunguka mradi huo hivyo kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji.
Alibaisha pia kuwa
Taasisi yake kwa kushirikiana na Kampuni ya Bakhresa inajenga kituo cha habari
katika mlango wa kuingilia eneo hilo ili kutoa taarifa na kuelimisha wananchi
kuhusu shughuli zinazofanyika katika eneo hilo ikiwa na pamoja na fursa
zilizomo ambazo wanaweza kufaidika nazo.
Hatua hiyo alisema ni
sehemu ya jitihada za kujenga maelewano mazuri na jamii ili kupunguza misuguano
kati ya wawekezaji na jamii.
Katika ziara hiyo Dk.
Shein alikagua ujenzi wa barabara kutoka Skuli ya Bwefum hadi Kiwanda cha
Maziwa cha Bakhresa yenye urefu wa kilomita 2.7 na upana wa mita 50 pamoja na
mtambo wa kupikia lami na mashine ya kusaga kokoto.
Barabara hiyo inajengwa
na Kampuni ya Ujenzi ya Coastal Dredging Company Tz Ltd ambayo ni kampuni tanzu
ya makampuni ya Bakhresa ambayo inajenga miundombinu katika mradi huo.
Kwa mujibu wa Mkurungezi
Mkuu wa Kampuni hiyo Ali Haroun Suleiman mtambo wa kupika lami una uwezo wa
kupika kati ya tani 100 hadi 110 za lami kwa saa wakati mashine ya kusaga
kokoto (crusher) ina uwezo wa kusaga kokoto tani 120 kwa saa.
Kampuni ya Bakheresa
tayari imejenga kiwanda kikubwa cha maziwa katika eneo hilo ambacho
kinasemekana ndio kiwanda kikubwa kabisa cha aina hiyo Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo Dk.
Shein alifuatana na viongozi mbali mbali wa serikali akiwem Waziri wa Ardhi,
Makazi, Maji na Nishati Mheshimiwa Ramadhani Abdalla Shaaban na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mheshimiwa Haji Omar Heri.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015,
Fax: 024 2231822
0 comments:
Post a Comment