May 05, 2014



















TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika kile kinachoonekana kuwa ni ishara nzuri kwa Bodi ya Mapato Zanzibar kuelekea kuvuka lengo la mwaka 2013/2014 katika makusanyo ya mapato iliyokadiriwa kukusanya na Serikali, kwa mara nyengine ZRB imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji kwa mwezi wa Machi.
Katika mwezi wa Machi 2014, ZRB ilikadiriwa kukusanya jumla ya TZS 15.96 bilioni kutoka katika vianzio mbali mbali inavyovisimamia. Na makusanyo halisi ya mwezi huo ni TZS 16.96 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 106.25 ya makadirio ikiwa ni kiwango kikubwa kuwahi kukusanywa kwa mwezi wa Machi tangu kuanzishwa kwa ZRB .
Kwa kulinganisha na makusanyo ya kipindi kama hiki cha mwezi wa Machi 2013 ya TZS 13.44 bilioni kunajitokeza ongezeko kubwa la makusanyo la  TZS 3.51 bilioni.
Miongoni mwa sababu zilizopelekea kuvuka lengo hilo la makusanyo kwa mwezi wa Machi ni kuimarika kwa msimu wa utalii Zanzibar pamoja na kufanyika kwa zoezi maalum la kugomboa madeni yanayotokana na kodi ya ardhi ambapo jumla ya USD 124, 502 sawa na TZS 203,360,770 ziliweza kugombolewa.
Kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na VAT na Ushuru wa bidhaa kutoka Tanzania bara sambamba ba zoezi la ukaguzi wa vyombo vya moto linalofanywa na Jeshi la Polisi limepelekea kufanya vizuri vianzio vya usajili wa vyombo vya moto na leseni za Udereva.
Hali ya makusanyo ya kodi kwa ZRB kwa kipindi cha miezi tisa (9) kuanzia July 2013 hadi kufikia Machi 2014 imekusanya TZS 134, 602, 492,842.73 bilioni ukilinganisha na makadirio ya TZS 133,924,978,461.00 bilioni sawa na asilimia 100.51, hali inayoashiria dalili nzuri kwa ZRB kuweza kufikia malengo ya ukusanyaji yaliyowekwa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.
Ili kufikia lengo hilo, ZRB inawaomba wananchi na wafanyabiashara waendelee kulipia kodi zao kama sheria inavyoagiza kwa madhumuni ya kuistawisha Zanzibar.
 
Makame Khamis Moh’d
Afisa Uhusiano
Bodi ya Mapato Zanzibar.
05/05/2014

0 comments:

Post a Comment