STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
15 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Mfuko wa Kimataifa wa
Maendeleo ya Kilimo(IFAD).
Dhamira hiyo amesema inatokana na ukweli
kuwa miradi inatekelezwa kwa ushirikiano na mfuko huo humu nchini inakwenda
sambasamba na utekelezaji wa Dira Zanzibar ya 2020 na Mpangomkakati wa Serikali
wa kuimarisha kilimo nchini.
Akizungumza na ujumbe wa Bodi ya Utendaji
ya Mfuko huo ulioongozwa na Dk. Yaya Olaniran Ikulu leo, Dk. Shein amesema
kwamba Serikali na wananchi wa Zanzibar wana matumaini makubwa na ushirikiano
na Mfuko huo kwa kuwa ushirikiano huo umekuwa wa manufaa makubwa kwa wakulima
wa Zanzibar.
“Azma yetu ni kuendelea kufanyakazi na
IFAD kwa kuwa malengo ya msaada wenu yanasadifiana na malengo yetu ya mipango
yetu mikuu kama vile Dira ya Maendeleo na Mpangomkakati wetu wa kuimairsha
kilimo ambayo yamelenga katika kujihakikishia usalama wa chakula na kuondoa
umasikini” alieleza Dk. Shein.
Katika mazungumzo hayo Mhe Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliueleza ujumbe huo kuwa
Serikali katika kuhakikisha wakulima wanapata huduma nzuri za kitaalamu imeamua
kuimarisha taasisi ya Utafiti ya Kizimbani hivyo ingependa kuona taasisi hiyo
inafaidika pia na misaada kutoka mfuko huo.
“Tumeamua kukipandisha hadhi kituo chetu
cha utafiti kuwa taasisi ili kutoa huduma bora zaidi kwa wakulima wetu na
katika eneo hili la utafiti tungependa kushirikiana zaidi na IFAD kukiwezesha
kituo kujenga uwezo kwa kukipatia mindombinu ya utafiti pamoja na
taaluma”alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa msaada
mkubwa kwa wakulima.
Aliueleza ujumbe huo kuwa binafsi anaamini
kama inavyoamini Bodi ya Mfuko huo kuwa ushirikiano huo una fursa ya kuleta
mabadiliko makubwa sio tu kwa wakulima bali kwa ustawi wa wananchi wote wa
Zanzibar.
“Nimefurahi kuwa ziara hii itawakutanisha
na wakulima wetu na kujiona wenyewe jinsi wanavyofanyakazi na kunufaika na
misaada ya IFAD na kwa hakika ni fursa pekee ya kuona namna Mfuko unavyoleta
mabadiliko kwa wakulima wetu”Dk. Shein alisema.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Bodi ya
Mfuko huo na uongozi wa IFAD kwa kufanyakazi kwa karibu na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kubainisha kuwa
uhusiano huo umekuwa wa manufaa kwa wakulima na jamii ya watanzania kwa ujumla.
Akitoa maelezo kuhusu ziara yao hiyo Kiongozi
wa Ujumbe huo Dk. Yaya Olaniran alisema kuwa ujumbe huo upo nchini kutembelea
miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Mfuko ambapo tayari wameshatembelea miradi
iliyo Tanzania Bara.
Alibainisha kuwa lengo la ziara hiyo ni
kuuwezesha Mfuko huo kujionea hali halisi ya miradi hiyo na kukutana wahusika
mbalimbali wakiwemo wakulima ambao ni walengwa wakubwa wa miradi hiyo.
“Kwa kutembelea miradi hii na kuona hali
halisi pamoja na kuzungumza na wakulima wadogo wadogo kujua ufanisi na
changamoto zake kutaisaidia mijadala katika Bodi na kufanya maamuzi
yanayoendana na uhalisia wa maendeleo ya miradi tunayoifadhili” alisema Dk.
Yaya.
Alieleza kuwa ushirikiano kati ya IFAD
Serikali zote mbili umekuwa mzuri na kwamba hadi sasa Mfuko huo umetumia dola
milioni 360 kusaidia wakulima katika miradi mbalimbali ya kilimo nchini
Tanzania.
“Miradi yetu imelekezwa katika sekta hii
ya kilimo ambayo inategemewa na wananchi wengi katika nchi zetu lengo ni kuinua
uchumi na kupunguza umasikini” alieleza na kufafanua kuwa IFAD inaamini kuwa
kufanya hivyo kutasadia pia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Miongoni mwa waliofuatana na Dk. Yaya ni
Katibu wa Mfuko huo Bwana Rasit Pertev, Mkurugenzi wa Mfuko huo Kanda ya
Mashariki na Kusini mwa Afrika Bwana Perin Sante Ange, Mwakilishi wa Mfuko huo
Tanzania bwana Francisco Pichon, Mkuu wa Programu kwa Tanzania Dk.
Mwatima Abdalla Juma pamoja na wajumbe wawili wa Ofisi
ya Tathmini ya IFAD.
0 comments:
Post a Comment