STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
16 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema
upanuzi na uimarishaji wa miundombinu ya usafari wa anga unaofanyika hivi sasa
umelenga kuhakikisha kuwa huduma za usafiri zinazotolewa Zanzibar zinakidhi
viwango vya ubora wa huduma hizo kimataifa pamoja kuzingatia viwango vya
usalama vinavyotakiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema hayo leo wakati akizungumza na
ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) ulioongozwa na
Katibu Mkuu wake Bwana Benjamin Raymond.
Aliuambia ujumbe huo kuwa huduma za
viwanja vya ndege na usafiri wa anga kwa ujumla, kama ilivyo kwa nchi nyingine
ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar na ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa nyakati tofauti kuimarisha sekta hiyo.
Alifafanua kuwa mwenendo wa usafiri wa
anga nchini unaonesha kuongezeka kwa abiria mwaka hadi mwaka ndio maana
Serikali imeamua kufanya upanuzi mkubwa wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Zanzibar na kwamba imo mbioni kuanza upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba ili
nao uweze kutoa huduma wakati wote.
“hivi sasa tunapokea watalii wapatao
200,000 kwa mwaka lakini matarajio yetu ni kufikia watalii 500,000 ifikapo
mwaka 2015 lakini hata hivyo baada ya upanuzi wa uwanja tunatarajia abiria
kuongezeka kufikia kati ya milioni 1.5 na milioni 2”Dk. Shein alifafanua.
Kwa hiyo alieleza kuwa ziara ya ujumbe huo
umekuja wakati muafaka kwa kuwa utapata fursa kuona jitihada za Serikali katika
kuimairsha sekta ya usafiri wa anga Zanzibar na Tanzania kwa jumla na kuongeza
ushirikiano kati ya ICAO na nchi yetu.
“Ziara yenu imekuja wakati huu muhimu
tunapopanua miundombinu ya uwanja wetu wa ndege wa Zanzibar na tungependa kuona
ICAO inasaidia kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa viwanja vyetu
ikiwemo kuijengea uwezo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na kutupatia vifaa
vya kutolea huduma katika viwanja hivyo kwa manufaa ya watumiaji wote wa
usafiri wa anga ”Dk. Shein alisisitiza.
Dk. Shein aliuhakikishia ujumbe huo ambao
ulijumuisha pia Mkurugenzi wa ICAO Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika
Bwana Mashesha Belayneh kuwa Zanzibar imejidhatiti kuhakikisha kuwa usafiri wa
anga unakuwa salama na wa raha wa watumiaji wake na ili kufikia lengo hilo ipo
haja kwa ICAO kuzidisha ushirikiano na Zanzibar.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la
Usafiri wa Anga (ICAO) Bwana Benjamin Raymond ameihakikishia Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana nayo katika
kuhakikisha kuwa hali ya usalama wa anga nchini unazidi kuimarika.
Amesema ujumbe wake umefika Zanzibar
kuangalia jinsi shirika hilo linavyoweza kushirikiana na Zanzibar kukabiliana
na changamoto zinaoendana na kupanuka kwa haraka kwa sekta ya usafiri wa anga
ikiwemo suala la usalama wa usafiri huo.
Alieleza kuwa kuna kila dalili za usafiri
wa anga kupanuka kwa haraka Zanzibar kutokana na kupanuka kwa sekta ya utalii
pamoja na uwekezaji unaovutia watu kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Kwa hiyo alieleza kuwa anaichukulia kwa
uzito mkubwa rai aliyotoa Mheshimiwa Rais ya kutaka shirika hilo kufanyakazi
kwa karibu na Serikali ya Zanzibar katika kusaidia kuimarisha usalama wa
usafiri wa anga nchini.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na
viongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano wakiongozwa na Waziri wake Mhe
Rashid Seif Suleiman,viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na
viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar(ZAA).
0 comments:
Post a Comment