May 16, 2014

Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD }umeombwa kuendelea kuunga mkono Sekta ya Kilimo Zanzibar katika njia ya kuwajengea uwezo wazalishaji wa Sekta hiyo mama ya uchumi  kupitia mfumo wa Teknolojia ya kisasa.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Serena Hoteli Shangani Mjini Zanzibar wakati wa dhifa maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya Ujumbe wa Bodi ya Utendaji ya Mfuko huo uliofanya ziara maalum kukagua miradi mbali mbali inayofadhiliwa na Taasisi hiyo ya Kimataifa.
Balozi Seif alisema Sekta ya Kilimo Zanzibar bado inaendelea kukabiliwa na changa moto kadhaa ambazo zinaweza kupunguwa iwapo msukumo wa Mfuko wa IFADI utaongeza kasi ya kitaalamu katika kusaidia sekta ya Kilimo Nchini.
Alielezea matumaini yake  kwamba juhudi zinazochukuliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza umaskini, njaa na kuongeza mara dufu uzalishaji wa chakula.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali kwa kushirikiana na Taasisi tofauti za ndani na nje ya Nchi imekusudia kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na matunda ili kuwapunguzia mzigo wananchi hasa wanaoishi sehemu za Vijiji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wajumbe wa Bodi hiyo Tendaji ya Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo kwa uamuzi wao wa kutembelea miradi inayoifadhili hapa Tanzania kitendo ambacho kitaongeza upeo wa ushirikiano kati ya Uongozi huo na Serikali zote mbili.
Mapema Mkuu wa Bodi hiyo yenye Makao Makuu yake Nchini Italy Dr.Yaya Olaniran alisema ujumbe huo ulipata fursa ya kuona hali halisi ya miradi mbali mbali inayofadhiliwa na mfuko huo pamoja na kukutana na wakulima ambao ndio wahusika wakuu wa miradi ya Mfuko huo.
Dr. Yaya alisema Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD } utaendelea kuunga mkono Serikali zote mbili Nchini Tanzania katika sekta ya Kilimo ikijikita zaidi katika kuwajengea uwezo wakulima pamoja na jumuiya za Kilimo ili zifikie hatua ya kujitegemea kiuzalishaji badala ya kusibiri misaada.
“ Ushirikiano wetu uliopo kati ya IFAD pamoja na SMT NA SMZ ndio sababu ya msingi iliyochangia Mfuko huo kuchangia harakati za maendeleo ya wakulima katika maeneo mbali mbali Nchini Tanzania “. Alisema Dr. Yaya Olaniran.
Naye Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD } Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika Bwana Perin Saint Ange akitoa shukrani kwa niaba ya Ujumbe huo alisema Visiwa vya Zanzibar vina rasilmali nyingi ambazo iwapo zitajengewa miundo mbinu imara zinaweza kunyanyua maisha ya Wananchi pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Bwana Perin alizitolea mfano rasilmali zilizomo ndani ya Bahari ya Tanzania kwamba zinafursa ya kukomboa maisha ya wavuvi wengi waliomo pembezini mwa bahari hiyo ambapo wengi kati yao hujishughulisha na kazi hiyo wakitumia vifaa duni visivyohimili masafa ya bahari kuu.
Dhifa hiyo fupi kwa Wajumbe wa Bodi Tendaji ya Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD } ilijumuisha pia baadhi ya Maafisa na watendaji wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment