SERIKALI ya Zanzibar imetiliana saini na kampuni
ya ‘JiangSu Provincial Construction Group Co. Ltd’ ya kutoka Jamhuri ya Watu wa
China, makubaliano ya ujenzi na utanuzi wa hospitali ya Abdalla Mzee iliyoko
Mkoani Pemba.
Hafla ya utiaji saini huo ilifanyika katika Wizara ya Afya,
ambapo Zanzibar iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk. Mohammed Saleh
Jidawi, wakati Naibu Meneja wa kampuni hiyo Dai Houxing alisaini kwa niaba ya
kampuni yake.
Akitoa shukurani kwa Serikali ya China, Dk. Jidawi alisema
hatua hiyo inadhihirisha kuimarika kwa uhusiano na udugu wa miaka mingi kati ya
China na Zanzibar, ambao umesaidia sana maendeleo ya visiwa vya Unguja na
Pemba.
Dk. Jidawi alisema ujenzi huo utaibadilisha kabisa
hospitali hiyo na kuwa ya kisasa zaidi ikiwa na huduma zote muhimu ikiwemo CT
Scan, chumba cha kuhifadhia maiti, jiko la kuchomea taka, idara ya maradhi ya
dharura, kitengo cha uangalizi maalumu (ICU), maabara na nyenginezo.
Aidha alisema, hatua hiyo itawezesha kuipandisha daraja na
kuwa hospitali ya rufaa kwa upande wa Pemba.
Alifahamisha kuwa kazi za ujenzi wa hospitali hiyo
zinatarajiwa kuanza mwezi moja tangu siku ya utiaji saini makubaliano hayo, na
umekisiwa kukamilika baada ya miezi 25.
Katibu Mkuu huyo alisema matengenezo hayo makubwa
yatagharimu dola za Kimarekani milioni 13, ambazo zote zitatolewa na Serikali
ya Jamhuri ya Watu wa China.
“Ni wazi kwamba hospitali ya Abdalla Mzee sasa imekuwa
ndogo kutokana na ongezeko kubwa la watu kulinganisha na wakati ilipojengwa
zaidi ya miaka 40 iliyopita,” alisema Dk. Jidawi.
Alisema makuabaliano ya kuifanyia matengenezo hospitali
hiyo yalitokana na ziara ya Rais wa China Mhe. Xi Jinping hapa Tanzania mwezi
Machi mwaka huu, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Halikadhalika alisema ziara ya Dk. Shein aliyoifanya mwezi
Mei 2013 nchini China, nayo imechangia pakubwa kwa nchi hizo kukubaliana kufanyika
kwa ujenzi huo.
Alizishukuru serikali zote mbili, pamoja na zile za Mkoa na
Wilaya ya Kusini Pemba, na watendaji wote wa wizara yake kwa kufanikisha
kufikiwa kwa hatua hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Yunliang ambaye alishuhudia utiaji
saini huo, alieleza matumaini yake kuwa kazi hiyo itafanyika kwa kiwango bora
kutokana na uzoefu mkubwa na wa miaka mingi ilionao kampuni ya JiangSu
Provincial Construction Group Co. Ltd ya China.
Alisema nchi yake inaona fahari kuendelea kuisaidia
Zanzibar ambayo imejenga nayo urafiki mkubwa tangu ilipojikomboa kwa Mapinduzi
ya mwaka 1964.
Naye Naibu Meneja wa kampuni ya JiangSu anayeshughulikia
miradi ya nje Dai Houxiang, aliahidi kuwa kazi hiyo itamalizika kwa wakati,
huku akiomba wananchi wa Pemba waipe ushirikiano kampuni yake wakati wote wa
ujenzi huo.
Alisema kampuni yake ina uzoefu wa takriban miaka 60 ikiwa
imefanya kazi katika nchi mbalimbali za Afrika na kujipatia umashuhuri mkubwa.
Hatua hiyo imekuja siku mbili tu baada ya China na
Zanzibar kusaini ujenzi wa kitengo cha uangalizi maalumu (ICU) katika hospitali
kuu ya Mnazimmoja.
0 comments:
Post a Comment