STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 18 Aprili , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kufanya utafiti wa kina kujua hali halisi ya tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabati na kutengeneza mpango mkakati wa kulimaliza kabisa tatizo hilo.
Dk. Shein amezungumza hayo wakati wa mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2013 na Machi 2014 ikiwa ni mfululizo wa vikao vya kujadili taarifa za utendaji kazi za Wizara za Serikali vinavyofanyika Ikulu.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo ni lazima utafiti wa kina ufanyike kuelewa mahitaji halisi ya walimu hao kwa kuainisha waliopo hivi sasa na walimu watarajiwa walioko vyuoni ili mpango wa kuongeza walimu hao kukidhi mahitajiutayarishwe na kutekelezwa.
Kwa kufanya hivyo alieleza kuwa tatizo hilo litaweza kutafutiwa suluhisho la kudumu kwa kushirikiana na taasisi za elimu nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Zanzibar –SUZA.
Katika kikao hicho Dk. Shein aliitaka Wizara hiyo kutoa elimu zaidi kuhusu mabadiliko yaliyofanywa na Serikali kupitia Baraza la Mitihani Tanzania-NECTA ya madaraja ya ufaulu ili kuepusha upotoshaji.
“ni muhimu jamii ikaelimishwa vya kutosha kuhusu mabadiliko hayo ili kusiwe na fursa kwa baadhi ya watu kulipotoshwa kwa makusudi suala hili” Dk. Shein alisisitiza.
Kuhusu kuimairisha huduma za maktaba Mhe Rais alisisitiza suala la maktaba kupatiwa majarida muhimu ya kitaaluma hasa yale ya sayansi ambayo ni muhimu katika kuwasaidia wanafunzi na watafiti katika fani zao.
Aliihimiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuharakisha maandalizi ya sheria ya kuanzisha Taasisi ya Elimu nchini ili chombo hicho muhimu katika ukuzaji wa elimu nchini kiweze kutekeleza majukumu yake.
Katika kikao hicho Dk. Shein alikumbusha na kusisitiza umuhimu wa michezo maskulini na kuielekeza Wizara, kwa sasa ambapo walimu wenye taaluma ya michezo ni wachache, kuweka mpango wa kuwa na walimu angalau wawili wa kuhamasisha michezo ambao watapewa mafunzo.
Wakati huo huo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imekamilisha ujenzi wa madarasa 118 yaliyoanzishwa na wananchi pamoja na kuzifanyia ukarabati skuli saba za msingi na nyumba nne za walimu.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo jana Katibu Mkuu Bi Mwanaidi S. Abdalla alieleza kuwa kati ya madarasa hayo 66 yako Unguja na yako 52 Pemba.
Sambamba na ujenzi huo alisema kuwa wizara imeweza kutengeneza na kuyapatia madarasa hayo mapya jumla ya madawati 1,800, viti 144 na meza 144. Aidha Wizara hiyo alisema ilipokea msaada wa madawati 100 toka kwa Benki ya NMB.
Kwa upande wa vitabu Bi Mwanaidi alieleza kuwa katika kipindi hicho jumla ya nakala 142,210 za vitabu vya wanafunzi na nakala za miongozo 3,820 ya walimu ilichapishwa.
Alifafanua kuwa vitabu na miongozo hiyo ambayo ni ya madarasa ya kwanza hadi la nne ya masomo ya Sayansi, Sayansi Jamii, Kiswahili na Kingereza ilianza kusambazwa maskulini mwezi Januari mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa wizara yake imeelekeza nguvu zake katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini kwa kuweka vipaumbele katika maeneo ya ongezeko la utoaji elimu na kuimarisha kiwango cha elimu inayotolewa.
Kwa minajli hiyo Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ya Juu ya Oman inaandaa programu ya mafunzo kazini kwa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi, hesabati na lugha ya kingereza katika ngazi ya sekondari ili kuwajengea uwezo zaidi walimu hao kumudu majukumu yao.
Pamoja na programu hiyo Bi Mwanaidi alisema mafunzo mengine ya aina mbali mbali kwa walimu yanafanyika katika vituo vya Ualimu ili kuongeza ufanisi kazini.
Sambamba na hatua hizo taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara tayari imeshakamilisha Rasimu ya Sheria ya Uanzishwaji wa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu ikiwa ni sehemu ya jitihda za kuhakikisha ubora wa kiwango cha elimu nchini.
Bi Mwanaidi alikieleza kikao hicho kuwa katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014 idara hiyo ya Ukaguzi wa Elimu ilikamilisha ukaguzi wa skuli 293 sawa na asilimia 86 ya lengo la mwaka.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
0 comments:
Post a Comment