Jamii imehimizwa kukitumia kipindi
hiki cha mvua za masika kupanda miti kwa wingi, ili kurejesha hadhi ya Zanzibar
ya kuwa "Visiwa vya Kijani".
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akizindua zoezi la upandaji miti
Kitaifa katika barabara ya Jendele Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kwa kiasi kikubwa jamii imepoteza
utamaduni wa asili wa kupanda na kutunza miti, hali inayopelekea kutoweka kwa
baadhi ya miti mikubwa ya matunda na viongo katika maeneo mbali mbali ya
Zanzibar.
Hivyo ameziagiza serikali za Mikoa na Wilaya
kusimamia utunzaji wa miti inayopandwa, ili kuhakikisha kwamba inakuwa vizuri
na kuleta ustawi uliokusudiwa katika utunzaji wa mazingira na kuongeza kipato
cha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema miti ina umuhimu katika uhifadhi wa
mazingira ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji vikiwemo chemchem na mito,
pamoja na kujikinga na upepo mkali, sambamba na kusaidia upatikanani wa mvua
ambayo ni muhimu kwa shughuli za kilimo na ustawi wa maisha ya binaadamu na
wanyama.
Ameongeza kuwa miti ni chanzo kikubwa cha pato la
wananchi na Taifa kwa jumla, akitolea mfano zao la karafuu ambalo ni miongoni
mwa vyanzo vikuu vya fedha za kigeni kwa Zanzibar.
Maalim Seif ametumia fursa hiyo kukemea tabia ya
baadhi ya watu kusafirisha miche ya mikarafuu nje ya nchi, pamoja na kuacha
kabisa matumizi ya misumeno ya moto ambayo ni adui wa mazingira.
"Nakuombeni wananchi tupande kwa wingi
mikarafuu na miti ya matunda pamoja na viungo, ili kuiweka nchi yatu katika
haiba nzuri ya kupendeza ambayo inaweza kuwavutia hata wageni wetu",
alisema Maalim Seif na kuongeza,
"Lengo la Serikali ni kupanda miti katika
barabara zote Unguja na Pemba, hivyo nakuombeni sana wananchi tushirikiane ili
kufanikisha lengo hili".
Kwa upande mwengine Maalim Seif amewataka
wafugaji kuheshimu juhudi za serikali na wananchi katika kuitunza miti hiyo,
ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za sensa
ya miti zinaonesha kuwa idadi ya miti inapungua kwa kiasi kikubwa ambapo maeneo
mengi ya misitu pamoja na mashamba yamegeuzwa kuwa makaazi ya watu na hivyo
kuendelea kukatwa kwa kasi.
Takwimu hizo zinaonesha kwamba katika mwaka 1997
visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa na miti yenye mita za ujazo wa 10.3
milioni, lakini kima hicho kilipungua hadi kufikia mita za ujazo 8.6 milioni
mwaka 2013.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili
Affan Othman Maalim, amesema jumla ya miembe 450 imepandwa katika uzinduzi huo
wa upandaji wa miti kitaifa, ambapo wanakusudia kuendeleza zoezi hilo katika
barabara yote ya Jendele hadi Unguja Ukuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kati bw. Vuai
Mwinyi amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa zoezi la upandaji miti tayari
limefanyika katika Wilaya za Kati na Kusini, na kuahidi kusimamia utunzaji na
uendelezaji wa miti hiyo.
Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipanda mti katika uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Kitaifa, katika eneo la barabara ya Jendele/Unguja Ukuu |
0 comments:
Post a Comment