April 27, 2014

Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imekukubali kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha michezo cha Mau Tse Tung kilichopo miperani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yunliang wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi huko  Mjini Dodoma.
Balozi Xie Junliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Timu ya wataalamu wa China inatarajiwa kukifanyia utafiti na uchunguzi kiwanja hicho baadaye mwaka huu sambamba na utiwaji saini Makubaliano ya ujenzi wa kiwanja hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao.
Alisema ujenzi wa uwanja huo uliopewa heshima ya Jina la Kiongozi muasisi wa Taifa la China Marehemu Mao Tse Tung utajumuisha kiwanja cha mchezo wa soka pamoja na michezo mengine ya ndani kama vile  Table Tennis.
“ Tunatarajia ujeni wa kiwanja cha Mao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanamichezo wa michezo tofauti ukiwemo ule unaopendwa zaidi wa soka “. Alisema Bwana Xie Junliang.
 Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Jamuhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika harakati zake za kujikwamua kiuchumi.
  Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jamuhuri ya Watu wa China kwa moyo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika miradi ya Kiuchumi na Maendeleo.
 Alisema mchango wa Serikali ya China kwa Zanzibar umesaidia kuiwawezesha asilimia kubwa ya Jamii Zanzibar kustawika Kijamii na hata kiuchumi kupitia miundo mbinu iliyowekwa na Serikali kwa msaada wa Nchi hiyo rafiki.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yunliang akiwasilisha agizo la Serikali yake kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi la kuridhia na kukubali kusaidia Ujenzi wa uwanja wa Michezo wa Mau Tse Tung uliopo Mtaa wa Mperani - Kikwajuni Mjini Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment