Wazanzibari wametakiwa kutokubali kuwaachia
watu wasioijua lugha ya Kiswahili kuiharibu, na badala yake wasimame kidete
kuilinda na kuiendeleza.
Akizungumza na washiriki wa maadhimisho ya
Siku ya Kiswahili Zanzibar yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha
Taifa (SUZA) Vuga, Rais mstaafu wa Tanzania Mhe. Ali Hassan Mwinyi, alisema
wakati umefika kuwaongoza wanaofanya makosa ya kimaandishi na matamshi katika
lugha hiyo.
Alifahamisha kuwa, katika siku za karibuni,
kumezuka mtindo wa kubadilisha maneno ya Kiswahili kutoka kwenye uasili wake na
kuyapopotoa.
Alitoa mfano wa baadhi ya watu kutamka nane
pahala panapostahili neno ‘manane, vinane au wanane’, mathalan kusema au
kuandika ‘watu nane’, matamishi ambayo si sahihi.
“Siku hizi imekuwa fasheni (mtindo)
kuyabadilisha maneno ovyo na hili hufanywa zaidi na watu wasiokifahamu
Kiswahili, lakini wenye lugha yao wapo na hawachukui hatua yoyote kuwarekebisha,”
alifafanua.
Mzee Mwinyi alisema visiwa vya Zanzibar ndio
shina la Kiswahili hivyo wananchi wake hawana budi kukitetea na kuhakikisha
kinashika nafasi yake kwa kuwaongoza wale wanaofanya makosa na kuwaelekeza
katika usahihi.
“Tusivunjike moyo, tuwafahamishe taratibu na
hatimaye watafahamu kwani papo kwa papo kamba hukata jiwe,” alisisitiza mwalimu
huyo mkereketwa wa lugha ya Kiswahili.
Katika hatua nyengine, aliziomba serikali zote
mbili za Zanzibar na Tanzania, kuwapatia mikopo wanafunzi wote wanaotaka kusoma
Kiswahili katika vyuo vya elimu ya juu, kwani wao ndio watakaokuwa watendaji wa
Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki ambayo makao makuu yake yameamuliwa
kuwa Zanzibar.
Pamoja na kuupongeza uongozi wa Baraza la
Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kwa uamuzi wake wa busara kuchagua siku ya
kuitukuza lugha hiyo, Mzee Mwinyi pia amewahimiza wananchi mbalimbali kununua
vitabu na majarida mengine yanayochapishwa na Baraza hilo, yakiwemo makamusi ya
lahaja za Kizanzibari ili kukisoma na kukijua vyema Kiswahili.
Aidha, aliziomba serikali zote mbili
kuzijengea uwezo taasisi zote zinazofanya kazi ya kukiendeleza Kiswahili ili
kiweze kusambaa kwa haraka kote ulimwenguni.
Mapema, Katibu Mtendaji wa BAKIZA Mwanahija
Ali Juma, alisema baraza hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali za
upotoshwaji wa Kiswahili unaofanywa kwa kisingizio cha maendeleo ya sayansi na
teknolojia.
Alisema miongoni mwa jitihada za BAKIZA katika
kuiendeleza lugha hiyo, ni kufanya utafiti wa lahaja kwa ajili ya kuandika
makamusi, ingawa kazi ya kuchapisha miswada hukwamishwa na ukosefu wa fedha.
Katika hafla hiyo iliyopambwa na shairi na
igizo yaliyokuwa na maudhui ya kukiimarisha Kiswahili na lahaja zake, mgeni
rasmi Mzee Ali Hassan Mwinyi alizindua jarida lililopewa jina la Jahazi, pamoja
na kukabidhi zawadi kwa mshindi wa kuandika tamthilia pamoja na washiriki
wengine wa shindano hilo.
Huu ni mwaka wa tisa tangu kuasisiwa kwa siku
ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili Zanzibar mwaka 2007, na ujumbe wa mwaka huu
ni ‘Sayansi na Teknolojia zitumike kuendeleza Kiswahili’.
:Maelezo Zanzibar
0 comments:
Post a Comment