Chuo cha Uongozi wa fedha Zanzibar (ZIFA)
kiliandaa ziara ya siku moja ya mafunzo kwa wakulima wa mwani wa Chwaka
kutembelea kikikundi cha Ushirika cha Tusife Moyo cha Kijiji cha Kidoti ambacho
kimepiga hatua kubwa katika kusanifu zao hilo kwa ajili ya matumizi mbali
mbali.
Ziara hiyo ni moja ya juhudi
zinazochukuliwa na chuo katika azma yake ya kusaidia jamii kufikia
maendeleo endelevu ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Mhadhiri wa ZIFA Maalim Said Mohd Khamis
alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar
mwaka jana, ulionyesha kuwa zao la mwani ambalo linawashirikisha asilimia 80
wananchi wanaoishi pembezoni mwa bahari, wengi wao wakiwa wananwake bado
halijamsaidia mkulima ipasavyo.
Alisema kutokana na kasoro hiyo chuo
kimeamua kutoa msukumo maalumu wa kutoa mafunzo ya vitendo kwa wakulima
wa mwani ili wawe na uwelewa wa kulisarifu zao hilo kwa matumizi mengine
badala ya kuwauzia wafanyabiashara kwa bei wanayopenda wao.
Maalim Said alisema wakulima wa mwani
wanatumia muda na rasilimali nyingi katika kushughulikia kilimo hicho
huku tija wanayopata ni ndogo na haikidhi nguvu wanazotumia.
Aliswashauri wakulima wa mwani wa Chwaka
kujikusanya na kuanzisha vikundi vya ushirikia ili waweze kupatiwa mikopo
na misaada ya kununulia mashine za kusarifu mwani kwa matumizi mengine kama
wanavyofanya wakulima wenzao wa kijiji cha Kidoti badala ya kuuza bidhaa hiyo
kwa bei ndogo.
Kikundi cha Tusife moyo cha Kidoti kinamiliki
mashine ya kutengenezea sabuni na mashine ya kusagia mwani mkavu kwa matumizi
mbali mbali ambapo kilo moja ya mwani uliosagwa inauzwa shilingi 10,000 na
kabla ya kusaga wanauza shilingi 300
Katibu wa kikundi cha Tusife moyo cha Kidoti
Hawa Simai Khamis aliwaeleza wakulima wa mwani wa kijiji cha Chwaka kwamba
mafanikio waliopata yanatokana na kujikusanya pamoja na kutafuta wafadhili wa
ndani na nje ya nchi
Amesema wanauweza wa kuzalisha aina tofauti za
sabuni na wamepata soko katika baadhi ya mahoteli ya kitalii yaliopo ukanda
wa Nungwi, Matemwe na Pwani Mchangani.
Katibu huyo aliongeza kuwa mwani kwa sasa ni
chakula na unatumika katika vyakula vingi ikiwemo mchuzi, keki , juisi,
kachumbari na pia unatumika kutibu maradhi mengi ikiwemo maradhi ya
ngozi.
Wakulima wa mwani kutoka Chwaka walifundishwa
kutengeneza sabuni na kupika mchuzi wa kukaanga kwa kutumia zao
hilo na kujifunza matumizi mengine .
Wakulima wa Chwaka walikishukuru Chuo cha
uongozi wa Fedha Zanzibar kwa kuwaandalia ziara hiyo na wameahidi kuyafanyia
kazi mafunzo waliyopata ili kuwa mkombozi wao kupitia zao la mwani.
Aidha walikishauri Chuo hicho kuendelea
kuwapatia mafunzo zaidi na kuwasimamia na kuwaongoza katika
kuanzisha ushirika wa mwani wa Chwaka.
0 comments:
Post a Comment