Makamu
wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw. Javier Rielo amemuhakikishia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa kampuni
hiyo itaanza ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha Mafuta kutoka nchini
Uganda hadi bandari ya Tanga hapa Tanzania haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha
za kutekeleza mradi huo zipo.
Bw.
Javier Rielo ametoa ahadi hiyo leo tarehe 14 Machi, 2016 alipokutana na kufanya
mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.Mradi huo utahusisha
ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi
kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na utarajiwa kuzalisha
ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Katika
Mazungumzo hayo Bw. Javier amemueleza Rais Magufuli kuwa Kampuni yake
inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari
zimeshaandaliwa.Pamoja na kuukaribisha uwekezaji huo mkubwa kwa Tanzania, Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza
kwa mradi, na ameshauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi huo
upunguzwe, ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.
Kwa
upande wake Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, amesema Wizara
yake ipo tayari kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, na itatoa ushirikiano wa
kutosha kuharakisha utekelezaji wake.
Prof.
Muhongo amebainisha kuwa licha ya kwamba hali ya kijiografia, hali ya hewa na
bandari ya Tanga vinatoa mazingira bora ya kufanikiwa kwa mradi huo, Tanzania
pia inatarajia kunufaika na bomba hilo, kwa kuwa kuna tafiti mbili za mafuta
zinazoendelea katika ziwa Tanganyika na katikati mwa Tanzania, ambazo zikikamilika
kwa mafanikio inatarajiwa bomba hilo litasaidia kusafirisha mafuta yake.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
14 Machi, 2016.
0 comments:
Post a Comment