Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao ili huduma zipatikane kwa wananchi kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa.
Amesema wakuu wa Mikoa na Wilaya ndio wenye dhamana katika Mikoa na Wilaya hivyo wanawajibika wa kusimamia utendaji kazi.
Amewataka kuwasimamia watumishi walio chini yao na kufanya nao kazi pamoja ili kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.
Rais wa Zanzibar amesema hayo alipokuwa akihitimisha mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ.
Amesema vikao vya kujadili utekelezaji wa Mipango kazi ya Wizara kama hicho ni muhimu kwani vinatoa fursa kwa viongozi wakuu na watendaji wa wizara kubadilishana uzoefu.
Mapema akitoa maelezo ya awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Heri amesema tangu kuundwa kwa wizara hiyo mwaka jana wameweza kuandaa mapendekezo ya muundo wa majukumu ya Ofisi, kukamilisha marekebisho ya rasimu ya Sera ya Serikali za Mitaa na kuchapisha Sera hiyo katika lugha ya kiswahili na kiingereza.
0 comments:
Post a Comment