Mkuu wa
Mkoa wa Kusini Pemba Mhe: Mwanajuma Majid Abdallah, amewataka wananchi Kisiwani
Pemba, kushirikiana kikamilifu katika kutokomeza vitendo vya udhalilishaji,
wanavyofanyiwa wanawake na watoto katika jamii.
Alisema kuwa, katika
kulitokomeza hilo ni lazima jamii iondoe woga na kuona haya, pia kuepusha
rushwa na vishawishi vyate ambavyo hukiuka haki na misingi ya kibinaadamu.
Mkuu huyo wa Mkoa
aliyaeleza hayo, wakati akizungumza na wananchi wa mikoa miwili ya Pemba,
katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, aliyofanyika katika uwanja wa
Gombani Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Aidha alisema hali
ya wanawake kwa sasa imejaa matatizo mengi ya aina mbali mbali ikiwa ni pamoja
na umasikini uliokithiri na uvunjaji wa Sheria zinazowahusu.
"Siku hii
wanawake hupata fursa ya kuangalia mafanikio na matatizo changamoto, Sote kwa
pamoja tunatakiwa kuwa makini na kusimamia kuondoa vitendo hivyo vionevu na
unyanyasaji wa mwanamke" alisema.
Alisema suala la
ukatili kwa wanawake hujumuisha mambo ya kupigwa, kufungwa, kubakwa, kukatwa
sehemu za mwili, kukatishwa masomo, kuozeshwa waume katika umri mdogo
kutumikishwa kusikokuwa na mipaka na kutojali utu.
Hata hivyo alisema
ni vyema kukumbusha vyombo vyote vinavyosimamia ustawi na haki za mwanamke
na watoto, hasa vyombo vya Sheria kusimamia na kuhakikisha vitendo vya
ushalilishaji vimepotea katika jamii.
Aidha alivitaka
vyombo vya sheria kusimamia vyema haki za wanawake na kuhakikisha wanastahili
kupewa haki zao wanapewa bila ya hofu yoyote.
Aliwataka wanawake
wenzake kuacha tabia ya kujidhalilisha wenyewe, wakati wanapofuata haki zao
wanapaswa kufuata taratibu, mila na desturi na silka za mzanzibari.
Hata hivyo aliwataka
wananchi, vyombo vya dola kushirikiana na kushikamana katika kuhakikisha
vitendo vyote vya udhalilishaji vinatokomezwa.
Naye mkuu wa Wilaya
ya Chake Chake Pemba, Mhe:Hanuna Ibrahim Masoud, aliwataka wanawake kujitokeza
kupinga vitendo vya udhalilishaji wanaovyofanyia majumbani na mitaani, ili
kuhakikisha wanaofanya vitendo hivyo wanatiwa hatiani.
Alisema tayari kuna
baadhi ya vijiji vimekuwa vikiwakandamiza wanawake, katika kupata haki zao
ikiwemo wanaume wanaokwenda agoni kukataa kupima afya zao wanaporudi majumbani
mwao.
“Mwanamme anakaa
miezi miwili au mitatu halafu akirudi akiambiwa kupima hataki, huu pia ni
udhalilishaji kwani hujuwi nini huko anachikifanya”alisema.
Kwa upande wake
Afisa Mdhamini wa Uwezeshaji Ustawi wa Jamii Vijana Wanawake na Watoto Mauwa
Makame Rajab, alisema wanawake ndio washiriki wakuu katika kuinua nchi yao
kiuchumi pia ndio walezi wa familia.
Alisema Serikali
imechukua juhudi kubwa ya kijenga Wizara, kuifanyia marekebisho Sera ya mwaka
2011 na kutaarisha vipindi mbali mbali ambavyo vinashajihisha kuleta maendeleo.
Alisema bado
wanawake wamekuwa wakikumbana na changamoto mbali mbali, ikiwemo Uwelewa mdogo
katika jamii, ikiwemo mambo ya sheria, urasimu katika majumbani, vyombo
vya sheria pamoja na baadhi ya sheria kuwa kandamizi ikiwemo sheria ya Ndoa ya
mwaka 1971.
Nae Ashloo Massoud
wakati alipokuwa akisoma Risala katika maadhimisho hayo alisema, wanawake bado
wanakabiliwa changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na uwezo mdogo wa
kujiendeleza elimu ya juu kwa wasichana, vitendo vya uzalilishaji, kukosa fursa
ya kumiliki ardhi na uchereweshaji wa kesi zinapopelekwa mahakamani.
Aliwaomba Viongozi
waunge mkono katika kuleta maendeleo endelevu katika jamii na kuwapa dhamana
wanawake katika ngazi mbali mbali kwa kuzingatia uwiano wa ajira.
0 comments:
Post a Comment