Waziri wa nchi afisi
ya Rais Ikulu zanzibar Dk. Mwinyihaji Mkame Mwadini juzi usiku alikuwa ni
miongoni mwa mamia ya Waandishi wa habari na wadau wa sekta ya habari Zanzibar
katika maziko ya aliyekua mwandishi na mtangazaji wa vituo mbali mbali vya
redio mjini Zanzibar Hafidh Hussein Mwinyi.
Hafidh maarufu Mpita Njia
alifikwa na mauti katika maeneo ya Maungani, wilaya ya Magharibi B Unguja baada
ya kupata ajali ya barabarani iliyohusisha vespa aliyokuwa akisafiria yeye na mpiga
picha wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Makame Mshenga na lori la mizigo
lililokua likitokea mjini kuelekea maeneo ya Dimani.
Katibu wa klabu ya
waandishi wa habari Zanzibar Faki Mjaka amesema msiba huo ni tukio la kushitua linalopaswa
kuwa na mazingatio makubwa kwa kila mwanadamu.
“Sio ZPC (klabu ya
waandishi wa habari Zanzibar) au familia pekee iliyoondokewa bali kila mmoja
miongoni mwa wapenda haki kwani marehemu alikuwa akiipenda kazi yake kiasi
wengi walikuwa wakimtabiria kuwa angekuwa miongoni mwa wanaharakati wakubwa
watakaoikomboa jamii kupitia fani ya habari”, amesema Mjaka.
Nae mtangazaji wa
kituo cha redio cha Coconut fm alichokuwa akifanyia kazi katika kipindi cha
coco jambo, anne Julius alikitaja kifo cha hafidhi kuwa ni pigo na pengo
litakalochukua muda mrefu kuzibika maoni yaliyoungwa mkono na mwandishi
mwengine Tabia Makame.
“Tulimtegemea kwa
uwezo alionao katika kujenga na kutetea hoja lakini pia ubunifu wake katika
utekelezaji wa majukumu yake, hakika ni pigo kwa kituo lakini mimi nadhani kifo
hiki kimenigusa zaidi kutokana na kuwa nilikuwa namtegemea zaidi katika kufanya
kipindi chetu kuwa bora”, amesema anne kwa huzuni kubwa.
Nae mwandishi wa
habari mwandamizi na mkufunzi wa mambo ya vyombo vya habari Ali Sultani
aliandika katika ukurasa wa ‘face book’ kuwa licha ya kukutana nae kwa mara ya
kwanza katika mkutano wa kujadili changamoto zinazowakabili waandishi wa habari
na vyombo vya habari wakati wa uchaguzi mchana wa Alhamis muda mchache kabla ya
kifo chake, amesema aligundua kuwa mwandishi huyo alikuwa na kipaji na uwezo
mkubwa wa kiuandishi.
“Awali sikuwa namjua
kabla ya kukutana nae leo(juzi) mchana kabla kukutwa na umauti, niligundua
uwezo na kipaji ambacho kingelimfikisha mbali katika fani hii”, ameeleza
mkongwe huyo ambaye alikuwa ni miongoni mwa watoa mada katika mkutano huo
ulioandaliwa na shirika la Inter News.
Mbali na kituo hicho
Hafidh kwa wakati tofauti alikuwa akifanya kazi katika vituo vya redio vya
Adhana FM na Mwenge FM ambapo pia alikuwa ni mwalimu wa fani ya uandishi wa
habari katika taasisi ya Mwenge Community Center inayomiliki kituo hicho cha
redio.
Maziko hayo ya
marehemu yaliyofanyika katika makaburi ya mwanakwerekwe yanatajwa kuwa ni ya
kipekee kutokana na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu licha kukamilika majira
ya saa saba usiku kutokna na mwili wa marehemu kuharibika vibaya kichwani baada
ya madaktari wa Hospitali ya Mnazi mmoja kushauri maiti hiyo izikwe kutokana na
kukosekana kwa mtambo wa ubaridi katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Wizara ya Uwezeshaji
Ustawi wa Jamii, vijana wanawake na watoto, imetoa mkono wa pole kwa
wanafamilia wote pamoja na wanahabari kwa msiba huo na kuwaomba kuwa na subra
wakati wote wakuomboleza.
Katika taarifa yake
imesema imepokea kwa masikitiko na mshtuko taarifa ya kifo cha mwanahabari Hafidh Hussein
Mwinyi kwa kuwa alikuwa mmoja kati ya wadau wa Wizara hiyo katika harakati za
mapambano dhidi ya udhalilishaji wa wanawake na watoto Zanzibar.
Marehemu Hafidh
alyezaliwa Februari 16, 1986 alipata elimu yake ya masingi na sekondari katika
skuli ya Mwanakwerekwe C Unguja kabla ya kujiunga na Mwenge Community Center
(MCC) kwa masomo ya uandishi wa habari katika ngazi ya cheti mwaka 2012 na akanza
kufanya kazi katika kituo cha redio cha
Adhana FM na baadae Coconut FM, alifanya vipindi maalum katika radio ya Mwenge
FM na alikuwa mwanachama wa klabu ya waandishi wa habari Zanzibar ZPC mwaka
2012.
MUNGU AMLAZE MAHALI
PEMA PEPONI AMIN
0 comments:
Post a Comment