STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
22 Februari, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM)wametakiwa
kujidhatiti zaidi kulinda na kuendeleza Mapinduzi ya mwaka 1964 na muungano
uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wito huo umetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa
CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa
Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) mkoa wa kichama wa Mjini Unguja.
Alibainisha kuwa kuyalinda na kuyadumisha
Mapinduzi na Muungano ni kulinda na kuendeleza amani na utulivu nchini hivyo
vijana hilo ndilo jukumu lao la msingi kama warithi wa taifa.
“hakuna mbadala wa Mapinduzi, hakuna mbadala
wa Muungano wala hakuna mbadala wa amani na utulivu wa nchi yetu hivyo ni
lazima vijana mchukue nafasi yenu kulinda misingi hiyo ya nchi yetu”
alisisistiza Dk. Shein
Alisema ni wakati wao vijana wa sasa kuchukua
majukumu hao kwa kuwa hata wao “walikuwa vijana kama nyinyi na tulihimizwa
kufanya hayo hayo na viongozi wetu na ndio maana tumefanikiwa kukabidhiwa
uongozi wa nchi yetu” Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao wa vijana kuanzia ngazi
ya matawi hadi mkoa.
Aliongeza kuwa ni lazima vijana wazingatie
“historia ya ukombozi wa nchi yenu na ya uongozi wake ndio mtaweza kuwa
viongozi wazuri na tegemeo la maendeleo ya nchi yenu”
Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliongeza kuwa vijana ni lazima wasome na
kukumbushana mara kwa mara historia ya mapambano ya Uhuru wa Zanzibar kwa
kuwa ni muhimu katika kujenga mustakbala wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Katika hotuba yake hiyo kwa vijana hao, Dk.
Shein alisisitiza kuimarisha umoja, maelewano na mshikamano miongoni mwa vijana
na kubainisha kuwa huo ndio msingi mkubwa wa mafanikio sio tu katika kutekeleza
majukumu yao katika chama bali pia katika kulijenga taifa.
Alihimiza vijana kujiepusha na vitendo
vinavyoweza kusababisha uvunjaji wa amani na utulivu na kuwataka vijana
kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kutetea na kulinda amani na utulivu
nchini.
Mkutano huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa
mikutano wa CCM mkoa wa mjini huko Amani ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
CCM hicho wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa
chama hicho.
0 comments:
Post a Comment