Serikali imesema
itaendelea kuimarisha mahusiano ya kideplomasia kati ya nchi rafiki na
wadau wa maendeleo ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025 na kutimiza malengo ya Mpango wa Maendeleo Endelevu wa Milinea (MGDs)
ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni hatua ya kuhakikisha inapunguza kiwango
cha umasikini na kuboresha maisha ya watu nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi
Dkt. Augustine Mahiga amesema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wakati
wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 iliyoshirikisha mabalozi mbalimbali
wanazoziwakilisha nchi zao Tanzania Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Hivi sasa Uchaguzi
Mkuu wa Tanzania Bara umekwisha. Ni wakati wa kufanya kazi na kauli mbiu yangu
ni “Hapa Kazi Tu”. Serikali mpya ya Awamu ya Tano imekuja na mkakati wa
kuboresha na kuimraisha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma ili kusisitiza
nidhamu na utendaji kazi, kuhesimu haki za binadamu, utawala bora na
kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania wanapata maendeleo
endelevu ya kiuchumi na kijamii,”amesema Balozi Mahiga.
Balozi Mahiga ameongeza
kwamba Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameiacha nchi ikiwa imara na marafiki wengi,
pia uchumi wake umekuwa katika kiwango cha asilimia saba (7) kwa kipindi cha
miaka mitano iliyopita.
Amesema mafanikio hayo
yametokana na juhudi za ushirikiano na misaada yao, hivyo aliwashukuru kwa
michango yao waliyoifanya hapa nchini.
“Ninawaomba muendelee
kutusaidia kwa kuwa hivi sasa tuna mipango ya maendeleo ambayo ina lenga
kuboresha maisha ya Watanzania wote hususan wale wanaoishi katika kiwango cha
chini cha umasikini,” amesema Balozi Mahiga.
Amezitaja changamoto zilizopo katika kutimiza malengo hayo ni
kuwepo kwa hali ya umasikini nchini, ukosefu wa ajira na rushwa. Hivyo Serikali
inafanya kila jitihada za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa bila ya
kufanya hivyo itakuwa ni vigumu kutimiza malengo ya nchi ya kufikia uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Balozi Mahiga amesema ili
kutimiza malengo hayo, Serikali inaendelea kudhibiti matumizi ya fedha zake,
kujenga nidhamu, uwazi na uwajibikaji katika matumizi hayo ndani ya Serikali na
hata kwa sekta binafsi na kuimarisha maeneo ya ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Serikali
imesema kwamba itaendelea kuendeleza ushirikiano huo, ili kuweza kupambana na
vitendo vya rushwa, biashara haramu ya binadamu, ugaidi na matumizi ya silaha.
“Tunawaomba mtusaidie
hasa kwenye eneo la upatikanaji wa taarifa, kujenga uwezo na masuala ya
kiufundi katika kukabiliana na vitendo hivi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu
suala la Uchaguzi wa Zanzibar, Balozi Mahiga amesema Zanzibar inajitegemea
katika masuala ya kisiasa na kiutamaduni licha ya kuwa ni sehemu ya Muungano wa
Tanzania.
Balozi Mahiga amefafanua
kuwa Zanzibar ina Katiba yake, Serikali na Tume Huru ya Uchaguzi .
Hivyo kutokana na
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 kufutwa kwa sababu mbalimbali
kama ilivyoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC).
Ameongeza kuwa mazungumzo ya
kufikia muafaka wa suala hilo, yanaendelea ma uchaguzi mwingine utafanyika
Machi 20, mwaka huu. Hivyo mazungumzo hayo bado yanaendelea ili kuufanya
uchaguzi huo uwe huru, haki na uwazi ili kukidhi viwango vya kimataifa vya
demokrasia.
Maelezo DSM
0 comments:
Post a Comment