December 15, 2015

Mkoa wa Mjini Magharibi bado unakabiliwa na ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu  wanaoripotiwa katika katika kambi ya wagonjwa hao iliyopo hospitali ya Chumbuni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Taarifa zinazema hadi sasa wagonjwa 30 wanaendelea kupatiwa matibabu  idadi iliyofikisha watu 342 walioambukizwa kipindupindu huku 7 kati yao wamefariki dunia tangu kuibuka ugonjwa huo mwezi Septemba mwaka huu.
Daktari dhamana  kanda ya Unguja Fadhil Mohamed Abdullah amesema asilimia 91 ya wagonjwa hao wanatoka katika shehia za Wilaya ya Magharibi  na shehia zilizoathirika zaidi ni Kiembesamaki, Mbweni, Kinuni, Kihinani, Fuoni na Tomondo.
Amewaambia wiongozi wa  Mkoa mjini magharibi na maafisa afya  kuwa  tafiti za wataalamu wa afya zimebaini asilimia 80 ya maradhi hayo yamesababishwa na wananchi kutumia maji ya kunywa yasiyo salama na vyakula vya majimaji vilivyoathiriwa na vimelea vya kipindupindu.

Ameomba mkoa huo kuwa na mikakati ya pamoja katika kukabiliana na mripuko wa maradhi ya kipindupindu hasa kwa kutolewa elimu zaidi kwa wananchi kuchemsha maji ya kunywa na kutia  dawa  maji ili kuyatokomeza kabisa.

Nao uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi umeahidi kuiendeleza mikakati  ya kukabiliana na maradhi hayo kwa kushirikiana na masheha  na kuangalia uwezekano wa kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula vya majimaji iwapo wananchi watendelea na kupuuza maelekezo yayotolewa na wataalamu wa afya.

0 comments:

Post a Comment