Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amekuwa mtu kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam la
kuhakiki silaha, ambapo bunduki zake mbili aina ya Shortgun na Pistol
zimehakikiwa nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es salaam.
Uhakiki huo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli
amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Jeshi la Polisi kwa kuendesha
zoezi la uhakiki wa Silaha, na ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha
nchi nzima kuhakikisha zinahakikiwa.Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi
kuongeza juhudi za kukabiliana na watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu
ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.
"Ni aibu kumuona askari polisi mwenye silaha ananyang'anywa
silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang'anye silaha na
wewe una silaha?" Amehoji Rais Magufuli.Kwa upande wake Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro, amemshukuru Rais
Magufuli kwa kuunga mkono zoezi hilo na amesema Jeshi la Polisi limejipanga
kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea kiti
cha Umeya katika Jiji la Dar es salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata Meya
katika uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho tarehe 22 Machi, 2016 badala ya
kuendelea kurumbana.
Dkt. Magufuli amesema upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya
uchaguzi huo, ili Meya apatikane na Jiji liweze kuendelea na mipango yake ya
kuwahudumia wananchi bila vikwazo.
"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya kweli" ameongeza Rais Magufuli
"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya kweli" ameongeza Rais Magufuli
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
21 Machi, 2016.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli
akiiweka silaha yake vizuri
mara baada ya kuhakikiwa
Ikulu jijini Dar es Salaam.
|
0 comments:
Post a Comment