
Alisema Serikali imetoa
kipaumbele cha kuongeza skuli katika Wilaya hizo mbili kutokana na ongezeko
kubwa la Idadi ya Watu ili zitakapomalizika zipunguze au kuondosha kabisa
msongamano wa wanafunzi uliopo hivi sasa kwenye skuli nyingi za Wilaya hizo.
Balozi Seif Ali Iddi
alitoa kauli hiyo wakati wa hafla maalum ya uzinduzi wa ujenzi wa Skuli
ya Sekondari ya Kwarara uliokwenda sambamba na uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha
Habari na mawasiliano cha Tumaini kwenye skuli hiyo hapo Kwarara Wilaya
ya Magharibi “B”.
Alisema kazi kubwa
iliyopo hivi sasa mbali ya kuongeza upatikanaji wa nafasi kwa wanafunzi ni
kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu wanayoipata wanafunzi kwa kuongeza
walimu wenye sifa zinazokubalika sambamba na kuboreshwa kwa maslahi ya walimu
hao.
Hata hivyo Balozi Seif
alisema ushiriki wa washirika wa maendeleo kuunga mkono jitihada za
Serikali ni muhimu na mazingira ya ushiriki wao tayari umeshaandaliwa vyema ili
waweze kutoa mchango wao wa elimu kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Alieleza kuwa sera ya
elimu ya mwaka 2006 imetamka wazi kwamba watoto wote wa Zanzibar wana haki ya
kupata elimu ya lazima kwa muda wa miaka 12, kuanzia elimu ya maandalizi,msingi
na ile ya elimu ya sekondari ya awali ya miaka minne.
Balozi Seif alisema
Serikali iliamua kufanya hivyo kwa kutambua maendeleo ya Taifa
yanayotegemea sana uwepo wa nguvu kazi ya Vijana walioelimika na ndio maana
awamu ya sita ya SMZ ikawekeza kwenye ngazi hizo kuanzia maandalizi hadi
sekondari.
Alisisitiza kuwa yapo
mafanikio makubwa yaliyopatikana akatolea mfano wa mwaka 2015 katika ngazi ya
elimu ya msingi wapo wanafunzi wapatao Laki 261,212 sawa na asilimia 98.4 ya
watoto wote wanaotakiwa kupata elimu hiyo.
Katika ngazi ya elimu ya
sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha Nne Balozi Seif
alisema wapo wanafunzi 84,211 sawa na asilimia 62.9 ya wanafunzi wanaotakiwa
kupata elimu husika.
Alieleza kwamba hayo ni
mafanikio makubwa yakujivunia kwa wananchi wote wa Zanzibar kwani hata baadhi
ya mataifa ambayo yana uwezo mkubwa wa kiuchumi kuliko Zanzibar lakini bado
hayajaweza kuwapatia elimu wananchi wake kwa asilimia kubwa kama iliyofikia Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliwapongeza wananchi kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao,
kwani pamoja na uhaba wa nafasi katika skuli mbali mbali lakini bado wamekuwa
na mwamko mkubwa wa kuwaandikisha watoto wao kwa wingi.
Alisema kwa vile Serikali
inatambua kuwa watoto ndio rasilmali muhimu kwa Taifa, rasilmali hiyo itaienzi,
itaitunza na kuiendeleza ili isipotee na kuwanasihi Vijana watakaopata fursa ya
kujiunga na skuli hiyo mpya ya Kwarara baada ya kukamilika waitumie nafasi pekee
ya kujijengea uwezo wa kujitegemea na kujikomboa.
Akigusia Kituo cha Habari
na Mawasiliano cha Tumaini kitakachojengwa kwenye skuli hiyo ya Sekondari
ya Kwarara Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amelipongeza Shirika la Habari la
Korea Kusini { Seoul Broadcausting System } kwa wazo lake la ujenzi wa Kituo
hicho.
Balozi Seif alisema
katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia matumizi ya vifaa vya
Habari na Mawasiliano vina umuhimu mkubwa katika utoaji wa elimu
hasa ndani ya karne hii ya 21.
Alisema Skuli ya
Sekondari ya Kwarara iliyobahatika mwanzo ndani ya Zanzibar kuwa na
mpango wa ujenzi wa kituo cha Habari kitakachokuwa na uwezo wa kurikodia
matangazo ya Redio na Televisheni kina muelekeo wa Dunia inavyokwenda hivi
sasa.
“ Nafuraha kubwa kusikia
kwamba Kwarara itakuwa skuli ya kwanza na ya aina yake hapa Zanzibar kuwa na
Kituo cha Habari na Mawasiliano na huo ndio muelekeo wa Dunia ya leo na ndio
hali halisi ”. Alisema Balozi Seif.
Aliushauri Uongozi wa
kamati ya Skuli utakaobeba jukumu la kuongoza skuli hiyo kuutaka kukitumia
kikamilifu kituo hicho cha Habari na Mawasiliano katika kuandaa vipindi mbali
mbali vya kufundishia wanafunzi sio tu kwa skuli hiyo bali pia kwa wanafunzi wa
skuli nyengine hapa Nchini.
Mapema Mwakilishi wa
Shirika la Good Neighbors Bwana Hwang Sungju, Mwakilishi wa Shirika la
Habari la Korea Kusini {SBS } Bwana Lee Woongmo pamoja na Mtendaji Mkuu wa
Shirika la Maendeleo ya Korea Kusini KOICA wamesifu mashirikiano makubwa
waliyoyapata kutoka kwa Wananchi wa Zanzibar.
Wawakilishi hao walisema
ushirikiano huo umesaidia kupatikana ufanisi mzuri wa mwanzo wa ujenzi wa
Skuli hiyo mpya na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ya elimu Nchini.
Walisema watendaji wa
mashirika hayo wanaelewa changamoto zinazowakabili wanafunzi wakati wa kufatufa
elimu hasa suala la umbali wa skuli unawasumbuwa baadhi ya wanafunzi hao.
Walieleza kwamba
changamoto hizo ndizo zilizosababisha mashirika hayo kuanzisha mradi maalum wa ujenzi
wa skuli za kisasa ulimwenguni wakielekeza zaidi nguvu zao katika bara la
Afrika.
“ Tumeshajenga skuli
zipatazo 100 katika nchi mbali mbali Barani Afrika ikiwemo Ethiopia, Kenya,
Chad, Malawi, Tanzania Bara na sasa hapa Zanzibar ”. Walisema wawakilishi wa
mashirika hayo.
Akitoa salamu Balozi wa
Korea ya Kusini Nchini Tanzania Bwana Song alisema uhusiano wa muda mrefu
uliopo kati ya Nchi yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla utazidi kuimarishwa
hasa katika sekta za Maendeleo ikiwemo ile muhimu ya Elimu.
Balozi Song alisema Korea
ya Kusini imefanikiwa kupiga hatua kubwa Kitaalamu hali ambayo imeamua
ujuzi huo kuutoa kwa kusaidia nchi marafiki hasa zile za Bara la Afrika.
Ujenzi wa Skuli ya
Ghorofa ya Kwarara pamoja na Kituo cha Habari na Mawasiliano uliowekwa jiwe la
msingi utakaokuwa na madarasa 12, maabara, Maktaba pamoja na huduma
nyengine muhimu unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 4 sawa na USD
za Korea Bilioni 1.6.
0 comments:
Post a Comment