Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji
Francis Mutungi ameviasa Vyama vya Siasa kushiriki chaguzi zinazotangazwa na
tume za uchaguzi nchini ikiwemo uchaguzi wa Machi 20, mwaka 2016 uliotangzwa na
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa kwa vyama
hivyo leo na kusainiwa na Jaji Mutungi ilieleza kwamba,
kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258 inasisitiza vyama vya
siasa kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa na tume za uchaguzi
ili kufikia malengo yake ya kushika dola.
“Katika nchi kidemokrasia na kwa chama cha
siasa kinachoamini misingi ya kidemorasia ya vyama vingi vya siasa, hakuna njia
mbadala kwa chama cha siasa kufikia malengo yake zaidi ya kushiriki uchaguzi.
“Ni wajibu wa kila chama cha siasa nchini
kama wakala wa kukuza demokrasia, utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa
kwanza kutii matamko ya kisheria yanayotolewa na mamlaka husika .
" Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki au
kimekwazwa kwa njia moja au nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya
uchaguzi, njia stahiki na inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea
uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za
uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.
Aidha Msajili huyo amesema kwa mujibu wa Sheria
za Nchi bado ni suala la hiari kwa chama kushiriki uchaguzi lakini utashi huo
wa hiari unaenda sanjari na umuhimu wa kila chama kushiriki kila uchaguzi
unaotangazwa na tume ya uchaguzi.
“Hivyo ni muhimu basi kila chama cha siasa
kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha siasa. Chama cha siasa
kisiposhiriki uchaguzi kinaua uhai wake katika mtazamo wa harakati za kisiasa,”alisisitiza.
Aliongeza kwamba hivi sasa, mfumo wa demokrasia
ya vyama vingi na vyama vya siasa vimeimarika, hivyo sio vyema kwa chama cha
siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa kutoshiriki uchaguzi wakati kina
uwezo wa kufanya hivyo.
0 comments:
Post a Comment