TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan leo amekutana na uongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba
Tanzania (WFT) ambapo amezungumzia dhamira ya serikali katika kuyatafutia
ufumbuzi matatizo mbali mbali yanayowakabili wanawake na watoto wa kike nchini.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais aliueleza ujumbe huo kuwa
wakati wa kampeni aliahidi pamoja na kazi za kumsaidia Mhe. Rais bado kama mama
atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi na
salama, kuboresha afya ya mama na mtoto, elimu na mazingira.
“Nilipokuwa kwenye kampeni nimejionea shida ya maji na wanawake
ndiyo wanaopata tabu ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji. Kwa hiyo, pamoja
na kazi zangu za kumsaidia Mhe. Rais nitasimamia miradi yote ya maji, alau
tuhakikishe maji yanapatikana umbali wa mita 400 kutoka eneo wananchi
wanakoishi au karibu zaidi”.
Alisema kinachofurahisha zaidi suala la maji liko kwenye Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na miradi mingi ikiwemo ya kuchimba visima virefu
katika mikoa kama vile ya Singida na Dodoma iko kwenye mchakato na cha msingi
ni kusimamia fedha zinatumika kuleta maji kama ilivyokusudiwa.
Kuhusu afya ya mama na mtoto alisema kazi hiyo ataianza hivi
karibuni kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za
wanawake ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mimba za utotoni.
“Hili tutajitahidi kulipunguza kwa kiasi kikubwa na hasa baada ya
serikali ya Awamu ya Nne kusema kwamba shule ya msingi ya lazima ni kutoka
darasa la kwanza hadi kidato cha nne”, alisema na kuongeza
“Katika kipindi hicho binti atakuwa amefikisha miaka 17, atakuwa
tayari kukabiliana na mambo ya uzazi tofauti na ilivyo sasa ambapo anamaliza
darasa la akiwa mdogo na matokeo yake anapata mimba katika umri mdogo. Mtusaidie
kupiga debe huko nje utekelezaji uweze kufanikiwa.”
Hata hivyo, alisisitiza kusimamia suala la kuhakikisha zahanati,
vituo vya afya na hospitali nchini zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha
katika wodi za wazazi kwa ajili ya kuhudumia akina mama na wananchi kwa ujumla
ambao wengi wanaonekana ni watiifu kwa serikali yao.
Kwa upande wa elimu Mhe. Samia alisema atasimamia ujenzi wa
mabweni kwa watoto wa kike na kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa sababu
uharibifu wa mazingira ndiyo umekuwa chanzo cha upungufu wa maji nchini.
Aidha aliuambia ujumbe huo kuwa hivi sasa tuna mpango wa
kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa ili
kinachopatikana kidogo kimfikie kila mwananchi.
“Tutaendelea kuaihirisha sherehe ili fedha hizo ziweze kutumika
kwa mambo ya kijamii. Kwa msimamo huu amabao Mhe. Rais ameanza nao labda watu
wote tushirikiane kwa kutatua matatizo yetu kwa gharama nafuu kwa ufanisi
mkubwa.”
Mapema akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Mtandao huo
Prof Ruth Meena alimpongeza Mhe. Samia kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi
akiwa mwanamke wa kwanza kuweka historia katika Tanzania.
Alimweleza Mhe. Makamu wa Rais matarajio yao kwa serikali ya Awamu
ya Tano kuwa itatetea misingi ya haki na usawa katika Nyanja zote.
x
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
24/11/2015
0 comments:
Post a Comment