May 08, 2014



www.zenjkijiwe.blogspot.com

JUMLA ya kesi 121 za udhalilishji zimeripotiwa katika kituo cha mkono kwa mkono (one stop centre), na Ofisi ya Ustawi wa Jamii, katika Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba kuanzia mwaka 2011 hadi Machi mwaka huu.
Kati ya kesi hizo, 84 zimeripotiwa ofisi ya ustawi wa Jamii wilayani humo kuanzia mwaka 2011hadi  mwezi Disemba mwaka 2013, ambapo kwa upande wa kituo cha mkono kwa mkono kimepokea kesi 37 za udahlilishaji kuwanzia mwezi Januari mwaka jana hadi Machi mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Afisa Ustawi wa Jamii, ambae pia ni Mratib wa kituo hicho Wete, Haroub Suleiman Hemed kesi hizo zilizoripotiwa ni pamoja na ubakaji (34), kulawiti(12), ujauzito(20), shambulio la aibu (7) pamoja na kutorosha (29) ambazo zimeripotiwa katika wilaya hiyo kuanzia mwaka 2011 hadi mwezi Machi mwaka 2014.
 Alisema shehia zilizoongoza kwa kuwa na matendo mengi ni shehia ya Kizimbani na Mchanga mdogo kesi 5, na shehia ya Kipangani na Mtambwe kaskazini zikiwa na idadi ya kesi nne.
Mratibu huyo alifahamisha kuwa, kati ya kesi zote ziliripotiwa kuanzia 2011 hadi 2012 na afisi yake ya Ustawi wa jamii, asilimia 75 hazikufikishwa mahakamani kutokana na kukosekana kwa kituo cha mkono kwa mkono wilayani humo .
Akizungumzia kuhusu kesi 37 zilizoripotiwa kituo cha mkono kwa mkono baada ya kuzinduliwa  mwaka jana, alisema kati ya hizo zilizofikishwa mahakamani ni kesi tano, nne zinasubiri uchunguzi wa vina saba ‘DNA’.
 Alisema kesi tisa (9) zimeishia polisi, sita (6) wahusika wamekubaliana, ambapo moja iko kwa DPP, huku saba (7) zikiendelea na kufanyiwa upelelezi  na Polisi.
Alisema kuwa, chanzo hasa cha matokeo hayo ni pamoja na  ukosefu wa maadili, malezi mabaya, umasikini, kutengana kwa wazazi, wazazi kutokuwa karibu na watoto wao pamoja na sheria inayosimamia matnedo hayo kukosa nguvu.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Elimu, Kijakazi Said Omar, Alisema kuwa, kuwepo kwa matendo hayo hupelekea athari mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuathirika kiakili kwa mtu aliyetendewa, maradhi ya zinaa, ukosefu wa elimu pamoja na kurejesha nyuma maendeleo ya jamii.
Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba  Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema matendo ya udhalilishaji wa kijinsia husababishwa na jamii kukosa maadili.
Alieleza kuwa hata suala la vijana kuiga mifumo na mwenendo ambao haimo ndani ya jamii ambayo wanaishi sambamba na kuwepo kwa ubaguzi katika malezi.
Kwa upande mwanafunzi wa skuli ya Chasasa Wete, Ummu-kheir Humud Rashid, alisema yeye anadhani kuwa suala la umaskini sambamba na mavazi yasiorasmi husababdisha ubakaji na wanawake kudhalilishwa.
Kadhi wa wilaya ya Wete sheikh Mohamed Ali Hamad alisema jamii kukiuka maadili ya dini yao, ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuwepo kwa udhalilishaji ndani ya jamii.
Mzazi Ali Hassan Kombo, alisema ili kuepusha mambo hayo, ni vyema jamii ikapatiwa elimu ya mara kwa mara ili kuwakumbusha jamii wajibu na jukumu lao kwa familia.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Wete Pemba, Omar Khamis Othuman alisema kuwepo kwa adhabu kali kwa wakosaji wa matendo ya udhalilishaji, ndio njia pekee ya kukomesha.
Baadhi ya wanaharakati wa kupambana na matendo hayo, walisema bado sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2004, imekuwa na mzunguruko mkubwa wa kupatikana ushahidi wa kesi za udhalilishaji.
Hivyo wameviomba vyombo vya sheria, kuwa makini wanapopata kesi za aina hiyo, ili wakosaji wapate adhabu kali na kukomsesha matendo ya udhalilishaji.    

0 comments:

Post a Comment