STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
8 Mei , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Sheria Namba 2 ya Utumushi wa Umma
ndio sheria mama za utumishi hivyo Taasisi na Wakala wa Serikali hazina budi
kuzingatia sheria hiyo katika masuala yote yanayohusu watumishi wake.
Amesema kuwa pamoja na kuwa taasisi na
wakala wa Serikali kuwa ni vyombo vilivyopewa mamlaka kujiendesha lakini bado
vinabaki kuwa vya serikali hivyo sheria ama kanuni za utumishi za taasisi hizo
hazina budi kwenda sambamba na Sheria hiyo.
Alifafanua kuwa mashirika na wakala wa
serikali wanatekeleza majukumu ya serikali ambayo Serikali yenyewe kwa sababu
mbalimbali imeamua au haiwezi kuzitekeleza kwa ufanisi au uhuru unaotakiwa.
Akizungumza katika mkutano uliojumushia
wenyeviti wa Bodi za Taasisi, mashirika na wakala wa serikali pamoja na wajumbe
wa bodi hizo Dk. Shein alisema lengo la kupitisha sheria hiyo ni kuhakikisha
kuwa utumishi Serikalini unakuwa bora na imara ili kuweza kutoa huduma stahiki
kwa wananchi.
Alibainisha pamoja na awamu zote za
Serikali zilizopita kufanya jitihada na kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha
utumishi serikalini lakini uzoefu unaonesha kuwa bado kuna udhaifu kwenye
utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu ya serikali.
“Tumekuwa tukifanya mageuzi kuimarisha
mazingira ya kazi kwa kuongeza nyenzo za kisasa na kuongeza maslahi ya
watumishi lakini tumeshindwa kufikia viwango tunavyo tarajia“ alieleza Dk.
Shein.
Alifafanua kuwa udhaifu huo unatokana na
usimamizi usioridhisha wa Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na kanuni zake
hivyo kuwafanya watumishi wengi kutozingatia nidhamu na kutotimiza wajibu wao
wawapo kazini matokeo yake ni kuzorotesha utendaji katika Serikali na taasisi
zake.
“Sheria zipo na kanuni zipo lakini mambo
hayaendi hivyo Serikali ya Awamu hii iliamua kuiweka Sheria Namba 2 ya Utumushi
wa Umma iliyopitishwa mwaka 2011 katika Katiba ili suala la utumishi wa umma
lipate msukumo wa kisheria na kutoa matunda yanayotarajiwa” Dk. Shein
alifafanua.
Kwa hiyo alitoa wito kwa wizara, taasisi,
mashirika na wakala wa serikali kuzingatia Katiba, Sera na Sheria ya Utumushi
wa Umma huku akitaka Kamisheni ya Utumishi wa Umma ambayo imeanzishwa kwa
mujibu wa sheria hiyo kupewa ushirikiano stahiki ili iweze kutekeleza majukumu
yake.
Dk. Shein alibainisha kuwa Kamisheni ya
Utumishi wa Umma ambacho ndicho chombo cha juu katika masuala ya utumishi wa
umma imekuwa ikikutana na vikwazo mbalimbali katika kutekeleza wajibu wake na
kuwataka viongozi na watendaji kutokiogopa chombo hicho kwani kiko kwa maslahi
ya nchi.
“Tuipe ushirikiano Kamisheni, haikuja
kuchukua wala kuingilia madaraka ya mtu bali kutekeleza matakwa ya kisheria
ambayo kila taasisi na kiongozi wake anapaswa kuyatekeleza” Dk. Shein
alisisitiza.
Kuhusu uhusiano kati ya bodi za taasisi za
serikali na wizara, Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
aliwaambia washiriki wa mkutano huo ambao ulijumuisha pia mawaziri na makatibu
wakuu kuwa ni wa lazima kwa kuwa wajibu wa Bodi ni kuishauri wizara.
“Lazima kuwepo mawasiliano ya karibu kati
ya Bodi na Wizara na kama kumetokea tofauti mazungumzo yafanyike kumaliza
tofauti hizo kwa faida ya nchi” Mhe Rais alisisitiza.
Mapema akitoa mada kuhusu Uhusiano baina
ya Utumishi wa Umma na Mashirika ya Serikali na Taasisi zinazojitegemea
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Othman Masoud alieleza kuwa uhuru wa mashirika
hayo ni wa kuyawezesha tu kuleta ufanisi lakini yanapaswa kuzingatia nguzo kuu
za serikali.
Alifafanua kuwa uwajibikaji wa Serikali ni
pamoja na mashirika na taasisi zake hivyo mashirika na taasisi hizo
zinatekeleza majukumu ya serikali na kuongeza kuwa Katiba inabainisha kuwa
watumishi wote wa taasisi hizo ni watumishi wa serikali.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee katika mada yake ya
Uongozi, Uwajibikaji, na Umuhimu wa Maadili katika Taasisi za Serikali
alitiliza mkazo juu ya viongozi na watendaji wakuu kuwa mfano katika
utendaji na kujenga utamaduni utakaopelekea kuleta ufanisi katika taasisi wanazoziongoza.
0 comments:
Post a Comment