Tume ya Haki za Binadadamu na
Utawala Bora Tanzania leo imezindua utaratibu mpya wa uwasilishaji wa
malalamiko na taarifa kuhusu uvunjwaji wa wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa wa misingi ya Utawala bora kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani
katika visiwa vya Zanzibar.
Akizindua mfumo huo katika Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar,
Kamishna Mkaazi wa Tume hiyo Zahor Juma Khamis amesema lengo la
mpango huo ni kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Amesema utaratibu huo unatarajia
kupunguza usumbufu na gharama kwa walalamikaji hasa wanaoishi
maeneo ya mbali katika kuwasilisha malalamiko yao katika ofisi za Tume na
kupata marejesho haraka.
“Itakumbukwa kuwa hapo awali
baadhi ya wananchi walilazimika kuacha shughuli zao za kiuchumi na kusafiri
hadi zilipo Ofisi za Tume ili kupata huduma hiyo, ”alisema Kamishna
Mkaazi Zanzibar.
Ameongeza kuwa utaratibu huo
utaharakisha mawasiliano kati ya Tume na walalamikaji kwa upande mmoja na
kati ya Tume na walalamikiwa, kinyume na utaratibu wa awali wa kutumia barua
kupitia Posta ambayo ilikuwa ikichukua muda mrefu na kukabiliana na changamoto
nyingi ikiwemo kupotea njiani.
“Utaratibu huu mpya sio tu unampa uhakika
mlalamikaji wa lalamiko lake kufika mbele ya Tume, bali pia unamuwezesha kupata
ushauri juu ya lalamiko lake ndani ya muda mfupi, ”alisisitiza Zahor Juma
Khamis.
Ameongeza kuwa utaratibu
huo utaongeza idadi ya malalamiko yanayowasilishwa Tume kutoka wastani wa
malalamiko mawili hivi sasa hadi 30 kwa mwezi na tayari wamejipanga kikamilifu
kuyashughulikia malalamiko yote ndani ya muda mfupi.
Kamishna Zahor amesema kwa
vile Tume inatambua kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa kutuma
malalamiko kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani hivyo imeandaa mkakati wa
kutoa elimu Tanzania nzima kuanzia mwezi ujao ili uweze kueleweka kwa wananchi
wote.
Awali Katibu Mtendaji wa Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi. Mary Massay amewataka wananchi hasa wanaoishi
mbali na Ofisi za Tume kuitumia nafasi hiyo kutuma SMS ya malalamiko yao na
hakuna malipo yeyote.
Amesema walengwa wakubwa wa
mpango huo ni wananchi wanaoishi vijijini ambao sio rahisi kuzifikia Tume
kuwasilisha malalamiko yao.
Utaratibu wa upokeaji wa taarifa
na malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wasimu ya kiganjani umefadhiliwa na
mpango wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa nchi zinazoendelea (SPIDER)
ya nchini Sweden.zenjkijiwe.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment