April 23, 2016

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema dhamira ya Serikali ni kuona watumishi wake wanapata maslahi mazuri zaidi ili kumudu gharama za maisha.
Pamoja na dhamira hiyo, hata hivyo, utekelezaji wake utategemea zaidi ukuaji wa uchumi ambao utatoa mapato zaidi kwa ajili ya kugharimia uendeshaji wa shughuli za serikali ikiwemo mishahara, alisema Dk. Shein.
Akizungumza na ujumbe wa viongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) ofisini kwake Ikulu jana, Dk. Shein alisema viongozi wa wafanyakazi wanapaswa kuelewa hali halisi ya mapato ya serikali na ugumu unaoambatana na kuongeza maslahi ya watumishi bila kuzingatia mapato halisi ya serikali.
“Sisi (serikali) wafanyakazi wametuchagua kuwaongoza na nyinyi (viongozi wa ZATUC) ni hivyo hivyo wamewachagua kuwawakilisha. Kwa hivyo ni viongozi kama sisi; hivyo wajibu wetu ni mmoja tu kuwatumikia wafanyakazi,” Dk. Shein alisema.
Rais Shein alitoa wito kwa viongozi wa ZATUC kuendelea na mashauriano na serikali mara kwa mara ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini na kuwapa taarifa mara kwa mara wafanyakazi juu ya hatua zinazofikiwa.
“Milango iko wazi, tuendelee kushauriana mara kwa mara isiwe karibu na ‘Mei Day’ tu," alisema Dk. Shein.
 "Wote lengo letu ni moja ambalo ni kuwatumikia wafanyakazi wenzetu.”
Aliutaka uongozi wa ZATUC kuendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali na kufuatilia hatua kwa hatua utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa wakati wa vikao vya mashauriano kati ya serikali na vyama vya wafanyakazi.
Dk. Shein aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma na kuahidi kuendelea kufanya kila jitihada kulipa malimbikizo ya madeni ya watumishi, ikiwemo malipo ya likizo.
Katika mazungumzo hayo ZATUC lilimpongeza Dk. Shein na serikali yake kwa kuimarisha maslahi ya watumishi na kuongeza fursa za ajira nchini.
“Tunazipongeza jitihada zako na za serikali unayoingoza kwa kuimarisha muundo wa utumishi wa umma na maslahi ya watumishi pamoja na kuongeza ajira nchini” Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohamed alisema.
Alibainisha kuwa ZATUC imefurahishwa sana na ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza mshahara wa kima cha chini hadi kufikia Sh. 300,000.00 kwa mwezi.

“Tunashukuru kuona kati ya mambo 12 tuliyozungumza katika kikao chetu cha tarehe 14 Aprili mwaka jana, mambo 10 yametekelezwa au yamo katika utekelezaji,” alisema Katibu Mkuu huyo.

0 comments:

Post a Comment