Kamishna hamdani amethibitisha kutokea kwa
mripuko huo wa bomu alioueleza kuwa ni sehemu ya mlolongo wa matukio ya
kihalifu yanayotokea Zanzibar, lilitokea majira ya saa 5 usiku bila ya kuathiri
maisha na kueleza kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanza.
Kiongozi huyo mkuu wa jeshi la polisi
Zanzibar, aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya jeshi
hilo visiwani humu, kuzungumzia hali ya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar
akirejelea matukio mbali mbali ya kihalifu Zanzibar yaliyotokea toka kufutwa kwa
uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana.
Matukio aliyoyarejea ni pamoja na mripuko wa
bomu uliotokea katika maskani CCM ya Kisonge, kuchomwa moto nyumba na majengo
taasisi za umma na kisiasa, kisiwani Pemba na uimarishawaji wa hali ya ulinzi na
usalama kuelekea katika uchaguzi mkuu wa marudio utakaofanyika baadae wiki hii.
“Katika kipindi hiki, kumetokea mambo mengi
yenye mnasaba na harakati za kisiasa na uchaguziujao, hivyo jeshi la polisi kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumeamua kuchukua hatua
madhubuti ili kuhakikisha tunadhibiti vitendo vyote vya kihalifu bila ya kujali
nani anaefanya au nani anaewatuma”, alisema Kamishna Hamdani bila ya kwenda
mbali zaidi kuhusu mripuko wa nyumbani kwake kwa kile alichodai kuwa hana
taarifa za kutosha.
Mripuko wa Bomu la maskani ya CCM Kisonge
Akizungumzia mripuko wa kisonge uliotokea
Machi 3 mwaka huu na kuathiri sehemu ya ofisi hiyo na baadhi ya nyumba za
karibu na eneo la tukio, kamishna Hamdani alisema uchunguzi wa awali umebaini
kuwepo kwa uhusiano kati ya bomu hilo na mengine yaliloripuka awali katika
maeneo tofauti.
“Uchunguzi wa kisanyansi wa tukio hilo bado
unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wote waliofanya kitendo hicho
na tunaahidi katika kipindi kifupi kijacho watuhumiwa hao watatiwa mbaroni na
kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria”, alisema kamishna huyo na kuwataka
wananchi kutokuwa na hofu ya wingi wa askari wa vikosi mbali mbali waliopo
nchini.
Uchomaji wa nyumba Moto wa Pemba
Akizungumzia matukio hayo ambayo yalitokea
jumamosi iliyopita ambapo nyumba 11 za makaazi ya wananchi, maskani 3 za CCM na
kituo cha afya kimoja vilichomwa moto na watu wasiojulikana katika mkuoa wa
kaskazini Pemba, Hamdani alisema jeshi lake limechukua hatua na kwamba hadi
sasa linawashikilia watu 31 kwa mahojiano.
Akijibu hoja kuwa kutokana na tukio hilo
polisi wamekuwa wakichukua hatua kali zaidi zinazowafanya baadhi ya wananchi
kukimbia makaazi yao, alisema tuhuma hizo sio kweli na kwamba watu
wanaoshikiliwa wanatokana na taarifa za kiintelijensia uliofuatiwa na msako
mkali wa jeshi hilo.
Mapema juzi chama cha wananchi cuf kupitia kwa
kaimu mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma Hamad Masoud Hamad
alisema katika kulishughulikia jambo hilo polisi wanatumia nguvu zaidi kiasi
cha kukiuka misngi ya haki za binadamu jambo ambalo kamishna hamdani
alilikanusha na kuwataka viongozi wa kisiasa kuacha kuchochea uwepo wa matukio
ya kihalifu.
“Polisi inafanya kazi kutokana na taarifa
inazokuwa nazo, hivyo kama kuna mtu anahusika na taarifa inayotufikia
hatutasita kumshughulikia au kuchukua hatua dhidi yake kwa kuwa huo ndio wajibu
wa msingi wa majeshi yote, sasa kama mtu hayataki haya asiwachochee wengine
kufanya uhalifu kwa kisingizio cha siasa”, alisema.
Hali ya ulinzi na usalama
Akizungumzia hatua ya kuimarishwa kwa hali ya
ulinzi na usalama katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kuelekea katika
kipindi hiki cha uchaguzi, kamishna hamdani alisema hali hiyo imelenga katika
kuwahakikishia usalama wananchi ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia na
kuwataka kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
“Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa pamoja
na kuwepo kwa viashiria vingi vya kihalifu, bado ulinzi utakuwa wa kutosha
kabla, wakati na baada ya uchaguzi kwani tumeamua kuongeza nguvu ya ulinzi
katika maeneo yote yanayotiliwa shaka ya kupangwa vitendo vya kihalifu”,
alisema.
Kuhusu matumizi ya wanajeshi katika baadhi ya
maeneo ya umma, Kamishna Hamdani alisema hilo ni jambo la kawaida kwa kuwa
majeshi yote yana lengo moja la kulinda katiba, mipaka ya nchi na usalama wa
raia na mali zao, na kwamba hatua hiyo inalenga katika kuongeza idadi ya
askari polisi katika doria na ulinzi wa mitaani.
"Majeshi katika nchi yeyote yana wajibu
mmoja wa kulinda mipaka ya nchi na katiba yake, usalama wa raia na mali zao
sasa kuna shida gani polisi wanapokabidhi baadhi ya majukumu kwa askari wa
vikosi vyengine? hili ni jambo la kawaida kwa raia wema ila kwa wale wenye
akili za kihalifu ni lazima walilalamikie kwani linawanyima fursa ya kutekeleza
uhalifu wao", alisema kamishna Hamdani.
Habari za kutokea mripuko nyumbani kwa
kiongozi huyo wa jeshi la polisi Zanzibar zilianza kuzagaa mapema asubuhi ya
jana huku askari polisi waliokuwa katika mavazi maalum kwa kushirikiana na
vikosi vya serikali ya mapinduzi Zanzibar vikionekana kuimarisha ulinzi katika
maeneo mbali mbali za mji wa Zanzibar huku kamishna huyo akiapa kuwashughulikia
wale wote watakaobainika kufanya uhalifu huo na mwengine uliotokea kabla.
0 comments:
Post a Comment