Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi hapa nchini Mheshimiwa Jaji
Damian Lubuva amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli kuwa tume hiyo ipo huru na haijawahi kuingiliwa kimaamuzi na
Rais wala kiongozi yoyote.
Jaji Lubuva amesema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam mara
baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ambapo alikuwa akimpa
taarifa juu ya yaliyojiri katika kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki
kilichofanyika Mjini Kampala, Uganda na kujadili kuhusu uchaguzi Mkuu wa Uganda
unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 mwezi huu.
Amesema katika kikao hicho ambacho yeye alikuwa mwenyekiti,
wamezungumzia umuhimu wa tume ya uchaguzi kuwa huru huku wakichukulia mfano wa
Tanzania ambayo imetoka katika uchaguzi mkuu miezi michache iliyopita.
Jaji Lubuva amefafanua kuwa tume ya uchaguzi inapaswa kuwa
huru katika maamuzi yake na kwamba jambo hili limekuwa likifanyika wakati wote
hapa nchini.
Amebainisha kuwa wanaosema Rais anapaswa kuingilia
kati masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya makosa, kwani
kwa namna yoyote Rais hana mamlaka hayo na hivyo hawezi kuingilia maamuzi ya
tume hizo
“Unaposikia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano aingilie hilo
suala la uchaguzi wa Zanzibar, yeye kwa kweli hana mamlaka kabisa. Pili ni kama
kujikanganya, huku unasema tuwe na tume huru isiyoingiliwa halafu huku unasema
aingilie kati maamuzi ya tume” alisema Jaji Lubuva
Jaji Lubuva amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kikatiba hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya tume ya uchaguzi ya
Zanzibar na hata huku bara pia hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya tume.
Mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi amewasihi Watanzania
kuwa uchaguzi umekwisha, na kuwaomba waungane na viongozi waliochaguliwa
kuchapa kazi ili kujiletea maendeleo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
Dar es salaam.
01 Februari, 2016
0 comments:
Post a Comment