Rais wa Shirika la Kimataifa lisilo la
Kiserikali linalosaidia Wananchi wenye kipato cha chini na wale wanaoishi
katika mazingira magumu {Dina Foundation} Runne Evardsen amesema mchango
uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuunga mkono taasisi
hiyo umewawezesha kutoa huduma za kibinaadamu kwa wananchi waliowengi Zanzibar.
Amesema mchango huo muhimu ulioleta faraja kwa
watendaji wa shirika hilo umewaongezea nguvu za kuendelea kutoa huduma hasa za
kiafya kwa wananchi wapatao Laki 150,000 kwenye shehia zipatazo 60 Unguja na
Pemba.
Evardsen amesema hayo akiuongoza Ujumbe wa
Viongozi Watano wa Shirika hilo la Dina wakati wa mazungumzo yake
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini
Zanzibar.
Amesema watendaji wa Dina hivi sasa
wanaendelea na mradi wa huduma za afya kwa kutumia gari Maalum ambapo
kila Jumamosi huzunguuka kwa hutoa huduma za matibabu bure kwa wagonjwa katika
maeneo tofauti.
Rais huyo wa Shirika la Kimataifa lisilo la
Kiserikali linalosaidia Wananchi wenye kipato cha chini na wanaoishi katika
mazingira magumu amefahamisha kuwa malengo ya baadaye ya Taasisi hiyo ni
kujenga kituo cha kudumu kama walivyofanya katika Nchi za Rwanda na
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya
Congo DRC}.
Ameeleza kuwa kazi hiyo imepangwa kwenda
sambamba na uimarishaji wa utoaji huduma nyengine za matibabu kama Meno pamoja
na kuwapatia msaada wa Baskeli Maalum Watu wenye ulemavu {Wheel Chair}.
Akitoa shukrani zake kwa huduma
zinazotolewa na Shirika hilo la Dina Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi amesema Serikali itaendelea kutoa ushauri na ushirikiano ili
kuona huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo zinawafikia Wananchi walio wengi hasa
Vijijini.
Amesema Mpango unaoendelezwa na Shirika la
Dina unakwenda sambamba na ile azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
kuwapatia huduma bora za afya Wananchi wake.
Katika kuimarisha sekta hiyo Balozi Seif amefahamisha
kuwa Sera ya Afya imetoa muongozo unaofahamisha vyema kuwa huduma za afya ya
msingi zipatikane katika masafa yasiyozidi Kilomita Tano.
Hata hivyo Balozi Seif ameueleza Ujumbe huyo
wa Shirika hilo kuwa zipo baadhi ya
changa moto zinazokwaza mpango huo lakini Serikali imejizatiti kuhakikisha miradi iliyoanzishwa
kwa ajili ya mpango huo inafanikiwa.
Balozi Seif ameipongeza Serikali ya Norway
kupitia Shirika hilo kwa jitihada inazochukuwa katika kuunga mkono harakati za
Maendeleo za Wananchi wa Zanzibar.
Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali
linalosaidia Wananchi wenye kipato cha chini na wanaoishi katika mazingira
magumu {Dina Foundation} lenye Makao Makuu yake Nchini Norway hutoa huduma
zote za afya ya msingi kutegemea mahitaji ya Wananchi wanaohusika.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
2/2/2016.
0 comments:
Post a Comment